Wafanyakazi wa sekta ya anga nchini Kenya wametishia kutatiza shughuli zote za usafiri wa anga iwapo matakwa yaoi hayatatimizwa na serikali
Kupitia chama chao cha wafanyakazi KAWU, wahudumu hao wametoa notisi ya siku saba kupatikana suluhisho, la sivyo wagome.
Notisi hii ya mgomo imetolewa baada ya kusambaratika kwa mazungumzo ya upatanishi yaliyoagizwa na mahakama, ikitaja matakwa muhimu ambayo hayajatatuliwa ikiwa ni pamoja na nyongeza ya mishahara iliyochelewa kwa muda mrefu.
Akihutubia waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa KAWU Moses Ndiema alisema imepita zaidi ya miaka 11 bila wafanyakazi kupata nyongeza ya mishahara, akishutumu Mamlaka ya Safari za anga ya Kenya, KCAA kwa nia mbaya katika kushughulikia maslahi ya wafanyakazi.
Alionya kuwa mamlaka zikishindwa kushughulikia matakwa yao ndani ya siku saba zijazo watalazimika kufunga kabisa anga ya Kenya.
"Tutafunga anga, kuzima kila kitu, na kufunga viwanja vyote vya ndege vya Kenya. Hili ni onyo. Ikiwa hawataingilia kati na kutatua masuala yetu ndani ya siku saba, tutachukua hatua," alisema.
Mgomo wa wafanyakazi wa anga utatatiza safari za ndege katika viwanja vyote vya Kenya, pamoja na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, na kusababisha pigo kubwa kwa utalii, biashara na usafiri wa anga wa kikanda.
Uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta pekee hushughulikia takriban ndege 117 za abiria kwa siku zinazoruka maeneo 38 duniani kupitia mashirika 27 ya ndege.












