Bao la kwanza katika mchezo lilitiwa kimiani na Aamir Abdallah Yunis katika dakika ya 6 ya mchezo na kuitanguliza Sudan mapema kabisa.
Wakati mashabiki wa soka ulimwenguni wakianza kufikiri kwamba huenda Sudan wakaushangaza ulimwengu wa soka kwa kuitoa Senegal katika hatua ya 16 bora, Senegal walitulia huku wakipanga upya mashambulizi wakisaka bao la kusawazisha.
Ikiongozwa na mchezaji nyota wao Sadio Mane, Senegal iliendeleza mashambulizi huku ikijilinda lakini ikionesha mchezo wa kushambulia zaidi.
Na katika dakika 29 tu mashambulizi haya yakazaa matunda pale Pape Gueye alipoachia shuti kali ndani ya boksi lililosmshinda mlina mlango na kujaa wavuni.
Baada ya bao hili la kusawazisha Senegal walionekana kurudi katika mchezo na katika dakika za nyongeza za kipindi cha awali kabla ya kwenda mapumziko Simba hao wa Teranga wakatia ‘chuma ya pili’ kupitia yule yule Pape Gueye.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi hasa upande wa Sudan kwani walianzisha mashambulizi ya kushtukiza na kufika langoni mwa Senegal mara kadhaa lakini Wasudani walishindwa kuzitumia vizuri nafasi walizozitengeneza.Dakika ya 77 ya mchezo mchezaji nambari 27 mgongoni Ibrahimm Mbaye, ambaye unaweza kumuita “super sub” akapigilia msumari wa tatu na wa mwisho katika nyavu za Sudan na kuzidi kudidimiza ndoto ya “vijana wa mto nile” kusonga mbele katika michuano ya Afcon.
Nyota wa Mchezo Pape Gueye amefunga magoli 2 na kuonesha mchezo mzuri wenye bidii na kujituma.
Mpaka kipyenga cha mwamuzi kinalia hapa kwenye dimba la Grand Stade de Tanger Mjini Tanger kikiashiria dakika 90 kumalizika, ubao wa matokeo ulisomeka Senegal 3-1 Sudan.


















