Kulingana na baadhi ya Watanzania mchakato mzima wa Uchaguzi huu unaonekana kughubikwa na ukosefu wa usawa kwa vyama vya siasa, mashaka juu ya uhuru wa taasisi muhimu, na migogoro inayotikisa msingi wa demokrasia ya vyama vingi.
Chama tawala – Chama Cha Mapinduzi (CCM) – kimeendelea kushiriki uchaguzi huo kikiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye anawania muhula wake wa kwanza kupitia njia ya kura.
Hata hivyo, mazingira mazima ya uchaguzi huu yameingia dosari, hasa baada ya chama kikuu cha upinzani, CHADEMA, kutangaza kutoshiriki uchaguzi, na mgombea wa ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina, kuondolewa kwenye kinyang’anyiro na Tume Huru ya Uchaguzi ya Tanzania (INEC) kufuatia pingamizi la Mwanasheria Mkuu wa nchi hiyo.
“Baada ya kuwa chama kikuu cha upinzani CHADEMA kutoshiriki uchaguzi na baadaye kuondolewa kwa mgombea wa Urais wa ACT Wazalendo Luhaga Mpina, uchaguzi wa Muungano (Tanzania bara) unakosa mvuto,” Odero Odero, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kiraia na Msaada wa Kisheria anaiambia TRT Afrika.
“Uchaguzi ni ushindani kama vile mpira, ili mechi ya mpira iwe na mvuto lazima timu zote mbili zitoshane nguvu,” Odero amesema, akimaanisha kuwa CCM inashindana na vyama dhaifu ambavyo haviwezi kulinganishwa nacho.
Kwa mujibu wa Odero, hali hiyo itaufanya mchakato huo kukosa mvuto na hata kusababisha watu kuupuzia mbali na hivyo huenda kukawa na wapiga kura wachache.
Hata hivyo, kulingana na Jawadu Mohamed, mchambuzi wa masuala ya kisiasa, uchaguzi wa mwaka huu bado una nafasi yake katika historia ya demokrasia ya nchi hiyo.
“Katika uchaguzi huu utaona kuwa kuna vyama 18 ambavyo vinashiriki, nusu ya vyama hivyo vimetoa wagombea wa nafasi ya Urais, ni chama cha ACT Wazalendo pekee, mgombea wake amepatwa na changamoto, na chama kingine kikuu ambacho ni cha upinzani CHADEMA hakina uwakilishi katika uchaguzi mkuu kwa sababu ya kukataa kushiriki kwao.”
Jawadu, hakubaliani na hoja kuwa mchakato wa mwaka huu, utapoteza uhalali wake kutokana na kutokuwepo na ushiriki wa CHADEMA.
“Kwa sababu lazima tukumbuke kwamba msingi wa demokrasia ya Tanzania ni mashina, unatoka chini kuelekea juu, sasa utaona ya kwamba vyama vingi vinavyoshiriki uchaguzi huu, vimejitahidi sana kuweka wagombea katika nafasi za udiwani, nafasi za ubunge, na baadhi ya vyama hivyo vina wagombea katika nafasi ya urais,” anasema Jawadu.
Historia ya utawala wa CCM na mfumo wa vyama vingi
Tangu ijipatie uhuru wake mwaka 1961, Tanganyika haijawahi kuongozwa na chama kingine zaidi ya CCM (awali TANU).
Ingawa mfumo wa vyama vingi ulirejeshwa mwaka 1992, wachambuzi wengi wa siasa wanadai kuwa mfumo huo umekuwa wa "vyama vingi kwa jina tu," huku vyombo vya dola, mahakama, vyombo vya habari, na hasa Tume ya Uchaguzi vikionekana kufungamana na chama tawala.
Rais Samia alichukua madaraka mwaka 2021 baada ya kifo cha ghafla cha Rais John Magufuli. Akiingia madarakani kwa ahadi ya mageuzi na kuimarisha demokrasia, wengi walitarajia mwelekeo mpya wa kisiasa. Kwa baadhi ya watu wanaona mwenendo wa maandalizi ya uchaguzi wa 2025 unaonyesha picha tofauti kabisa.
“Ni dhahiri ya kwamba CCM ina nguvu na ushawishi kuliko vyama vingine, na hili halitokani kama wanavyodhani wengi kwamba labda pengine kupendelewa na mifumo ya dola, lakini kubwa ni misingi ya chama chenyewe, watu watakumbuka kwamba chama hichi kina zaidi ya miaka 48, ni chama ambacho kina nasaba na ukombozi wa bara la Afrika, kina nasaba na kupigania haki kwa muda mrefu, kimejijenga kwa muda mrefu katika eneo la raslimali ya wanachama, kimejijenga kwa muda mrefu katika raslimali ya fedha, na kina msuli,” ameelezea Jawadu.
Jawadu ameongeza kusema, “CCM ina wanachama zaidi ya milioni 13, pamoja na wapenzi wa chama hicho na wingine ambao hawana kadi za uanachama, wanapindukia karibu milioni 30. Hao wote wana imani na mchakato unaoendeshwa na Tume.”
Amesisitiza kwamba, vyama vya siasa vya Tanzania vinahitaji kuwekeza muda zaidi katika vyama vyao na kutafuta ushawishi kutoka kwa wananachi na sio kujitokeza tu wakati wa uchaguzi kutafuta kura.
Hata hivyo Odero ameonesha kutokuwa na imani na demokrasia ya Tanzania, akisema kuwa kulingana na katiba ya Tanzania ibara ya 3, Tanzania ni nchi inayofuata demokrasia. Anasema kuwa linapokuja suala la utashi wa kisiasa, demokrasia bado iko nyuma.
CHADEMA yagomea uchaguzi
Mnamo Aprili 12, 2025, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ilitangaza kuwa CHADEMA haitaruhusiwa kushiriki uchaguzi wowote hadi mwaka 2030 kwa kosa la kukataa kusaini Kanuni ya Maadili ya Uchaguzi.
CHADEMA waligoma kusaini kanuni hiyo kwa madai kuwa hakuna mabadiliko ya msingi yaliyofanyika katika mfumo wa uchaguzi. Miongoni mwa masharti yao ni:
Kuanzishwa kwa Tume Huru na yenye uwajibikaji wa kweli;
Mahakama kupewa mamlaka ya kupitia matokeo ya uchaguzi wa urais;
Kurudishwa kwa mchakato wa Katiba Mpya.
Kwa sasa, kiongozi wa CHADEMA, Tundu Lissu, anakabiliwa na mashtaka kadhaa ikiwemo ya uhaini kufuatia matamshi yake ya kutaka mageuzi ya kikatiba.
Hata hivyo, Odero ameikosoa hatua ya CHADEMA kutoshiriki uchaguzi hadi pale mabadiliko yatakapofanyika, kulingana na yeye amesema, “haikua jambo la busara CHADEMA kumsusia mtu ambae hana hata chembe ya aibu, dawa yake ilikuwa kupambana naye”.
Amesema sasa CHADEMA iko katika wakati mgumu, kwa sababu vyama hua vinategemea ruzuku, na sasa CHADEMA itakosa ruzuku, na pia kukosa wabunge na hata madiwani kwa sababu ya kutoshiriki uchaguzi na hivyo kuatihiri uwezo wao wa kifedha hata katika uchaguzi ujao.
Na kwa mujibu wa Jawadu, “Hata kama CHADEMA ingeshiriki, bado uwezo wa CCM ungelikuwa ni mkubwa zaidi. Ni mwaka huu tu ambao CHADEMA imeamua kutoshiriki, lakini kwa miaka mingine iliyopita walishiriki, ni dhahiri kwamba hawakua wanashinda, kwa nini hawakua wanashinda, kwa sababu, walikuwa wanashindana na chama chenye misingi ne chenye kujijenga zaidi”.
Luhaga Mpina na Sakata la Mgombea wa ACT-Wazalendo
Katika tukio jengine la kutatanisha, aliyekuwa Waziri wa Mifugo na Mbunge wa CCM, Luhaga Mpina, alijiunga na ACT-Wazalendo mnamo Agosti 2025 na kuteuliwa kuwa mgombea wa urais. Hata hivyo, uteuzi wake ulizua mvutano mkali ndani ya chama na kwenye Tume ya Uchaguzi.
Mwanachama mmoja wa ACT aliwasilisha pingamizi kuwa Mpina alijiunga na chama siku moja kabla ya kuteuliwa, jambo ambalo linakiuka kanuni za chama. Kutokana na malalamiko hayo, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ilipoleka pingamizi INEC, Tume hayo ililikubalia pingamizi hilo na hatimae kumzuia kuwasilisha fomu mnamo Agosti 27.
Mnamo Septemba 11, Mahakama Kuu ya Tanzania ilitengua uamuzi wa Tume na kusema kuwa Mpina alinyimwa haki ya kusikilizwa.
Hata hivyo, saa chache baadaye, Tume hiyo ilimwondoa tena Mpina kufuatia pingamizi jipya lililotolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari.
Odero amesema, “Tanzania tuna shida kwenye mfumo wetu wa uchaguzi, na mfumo wenyewe umejengwa mbali sana na katiba.” Akisema kuwa Rais wa Tanzania ana mkono mrefu sana, yeye ndio anateua tume ya uchaguzi na hivyo kufanya watu kukosa imani na tume hiyo.
Odero anaendelea kusisitiza kwamba, kilichomuondoa Luhaga Mpinga kwenye uchaguzi, ni kuwekewa pingamizi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Odero anasema, “Kwa lugha nyengine nyepesi, ni kuwa Rais Samia ndie aliemuekea Mpina pingamizi kwa kutumia mtumishi wake anayeitwa mwanasheria mkuu wa serikali.”
Kwa upande wa Jawadu, “Hoja za kumuondoa Mpina kama mgombea wa Urais si za kutunga, zina yakini na haki ndani yake, na kupitia hoja hizo, ndio zilizomtoa mgombea Mpina, na sasa kama tunaamini katika sheria na kanuni, ni vigumu sana kuamini kuwa Mpina ameonewa, ameondelowa na sababu za kisheria ambazo zilikuwa wazi na watu nchi nzima walizisoma”.
Mtazamo wa Jumuiya ya Kimataifa
Sakata la Mpina na kutoshiriki kwa CHADEMA limezua maswali mazito kuhusu uhuru na uadilifu wa vyombo vinavyosimamia uchaguzi. Watetezi wa haki za binadamu na wachambuzi wa siasa wanasema kuwa sheria na taratibu zimekuwa zikitumika kwa njia za upendeleo, huku vyama vya upinzani vikizuiwa kwa visingizio vya kiutaratibu.
Kwa kipindi kirefu, jumuiya ya kimataifa ilionekana kusita kuchukua msimamo wazi. Hata hivyo, hali hiyo imeanza kubadilika. Mnamo Mei 2025, Bunge la Ulaya lilipitisha azimio kulaani hatua ya kuizuia CHADEMA kushiriki uchaguzi, pamoja na mashtaka dhidi ya Tundu Lissu.
Waangalizi kutoka Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya, na mashirika ya kiraia wanatarajiwa kufuatilia uchaguzi huo kwa karibu.
Kutokuwepo kwa CHADEMA — chama kikuu cha upinzani chenye historia ya kukosoa na kupambana na mfumo serikali, kunafanya uchaguzi huu kukosa mvuto wa kidemokrasia. Wengi wanaamini kuwa wapiga kura huenda wakakata tamaa na kutoshiriki, wakiamini kuwa matokeo tayari yamepangwa.
Lakini Odero ana maoni tofauti, “Jumuiya ya kimataifa ni watu wenye maslahi na yule mwenye kuwapa kitu, hawana maslahi na watu ambao hawawapi kitu, watapiga kelele hapa na pale kama sehemu ya kutuliza joto la nchi lakini baadaye watakaa meza moja. Kwa sababu wanafaidi na madini na raslimali zetu, kwa hivyo usitegemee Ujerumani au nchi nyingine kama zitakuja na shinikizo kubwa kutaka uchaguzi urudiwe.”
Naye Jawadu amesisitiza kuwa, Jumuia ya kimataifa imekua ikiuchukua upande bila ya kufanya utafiti wa kina juu ya mambo wanayoyasimamia. Ridhaa ya mamilioni ya wapiga kura ni muhimu zaidi kuliko ile ya jumuiya ya kimataifa.”