Mpishi maarufu wa Nigeria Hilda Effiong Bassey, ameingia kwenye vitabu vya rekodi za dunia za Guinness baada ya kufanikiwa kupika kiwango kikubwa cha wali aina ya Jollof, ambao ni mlo maaurufu nchini Nigeria.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa siku ya Jumatatu, mpishi huyo, ambaye anatambulika kwa jina maarufu la Hilda Baci, aliweka rekodi hiyo akiwa katika eneo la Victoria Island jijini Lagos, baada ya kufanikiwa kupika wali wenye kilo 8,780.
Kulingana na waandaaji wa onesho hilo, ambalo lilifanyika Septemba 12, 2025 upishi wa chakula hicho, ulichukua masaa 9, ukihusisha kilo 220 za nyama ya kuku, kilo 164 za nyama ya mbuzi na kilo zaidi ya 600 za pilipili.
Upishi wa mlo huo ulifanyika ndani ya chombo chenye ujazo wa lita 22,000, ukitumia nishati ya gesi ya zaidi ya kilo 1,200 ndani ya saa tisa.