| Swahili
AFRIKA
3 dk kusoma
Watoto watekwa nyara Nigeria
Kanisa Katoliki na Jumuiya ya Kikristo ya Nigeria linasema wanafunzi 50 kati ya zaidi ya 300 waliotekwa nyara kutoka shule ya Kikatoliki ya Nigeria wametoroka na kuungana na wazazi wao.
Watoto watekwa nyara Nigeria
Zaidi ya watoto 300 walitekwa nyara katika shule ya Kikatoliki Papiri, Nigeria
24 Novemba 2025

Kuna hali ya Sintofahamu nchini Nigeria ambapo watoto wa shule wametekwa nyara. Hili lilitokea katika Jimbo la Niger, eneo la kaskazini kati la Nigeria ambapo wanafunzi zaidi ya 300 katika shuler ya Kikatoliki walivamiwa na kutekwa.

Rais wa Nigeria Bola Tinubu ameagiza kuajiriwa kwa maafisa 30,000 zaidi wa polisi na kuamuru kuondolewa kwa polisi wote walio katika majukumu ya kulinda viongozi kurejeshwa katika majukumu yao ya msingi.

Anataka maafisa zaidi wapelekwe katika maeneo ambayo raia wanashambuliwa na watu wenye silaha.Haya ni matukio mabaya zaidi ya utekaji nyara tangu kutekwa kwa wasichana 276 wa Chibok na Boko Haram kaskazini mashariki mwaka 2014. 

Kanisa Katoliki na Jumuiya ya Kikristo ya Nigeria linasema wanafunzi 50 kati ya zaidi ya 300 waliotekwa nyara kutoka shule ya Kikatoliki ya Nigeria wametoroka na kuungana na wazazi wao.

Lakini karibu watoto 253 waliotekwa nyara, pamoja na wafanyakazi 12 na walimu, bado wamezuiliwa na watekaji.

Utekaji nyara huo ni wa hivi punde zaidi katika mfululizo wa mashambulizi dhidi ya shule ambao umelazimu baadhi ya majimbo ya kaskazini kufunga shule. Serikali pia iliagiza kufungwa kwa vyuo 47 kaskazini mwa nchi hiyo.

Siku ya Jumapili kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Leo aliomba kuachiliwa mara moja kwa wale ambao walikuwa wametekwa katika moja ya matukio mabaya zaidi ya utekaji nyara kuwahi kutokea nchini Nigeria.

Lakini ni nini kinachochea mashambulizi haya?

Wataalamu wanasema mashambulizi hayo yanafuatwa mfumo mahsusi.

Magenge yanayojulikana ya wavamizi wenye silaha, hufyatua risasi mara kwa mara ili kuwatisha watu, kuwateka nyara waathiriwa na kukimbilia kwenye misitu iliyo karibu. 

Serikali ya Nigeria imekataa kuhusisha utekaji nyara huo na mateso dhidi ya Wakristo kama alivyodai rais wa Marekani Donald Trump.

Watu hao waliokuwa na silaha walivamia shule ya wasichana yenye Waislamu wengi kaskazini magharibi mwa jimbo la Kebbi na kuwakamata wanafunzi 25.

Pia genge lingine lililokuwa na silaha liliwateka nyara watu 64, wakiwemo wanawake na watoto, kutoka katika nyumba zao jimbo la Zamfara, linalopakana na Kebbi.

Watu wenye silaha walishambulia kanisa la Christ Apostolic katika jimbo la kati la Kwara na kuua watu wawili na kuwateka nyara waumini 38.

Maafisa walisema watu hao wenye silaha walikuwa wanadai kikombozi cha naira milioni 100 (takriban $69,000) kwa kila mtu.

Wataalamu wa usalama wanasema mashambulizi hayo na utekaji nyara huchochewa na tamaa ya kupata pesa, na shule ni rahisi kulengwa kwani hazina usalama wa kutosha. Pia, wazazi wako tayari zaidi kutafuta fedha za kikombozi ili kuwapata watoto wao.

Sehemu kubwa ya kaskazini mwa Nigeria, inayojumuisha zaidi ya majimbo 20 kati ya majimbo 36 ya nchi hiyo, imegubikwa na ukosefu wa usalama, na kutatiza maisha ya kila siku ya watu, ikiwa ni pamoja na usafiri na kilimo.

Upande wa kaskazini-magharibi, magenge yenye silaha yasiyo na malengo yoyote ya kidini au kisiasa huteka nyara na kujificha kwenye misitu. Nigeria ina maeneo makubwa yaliyo wazi na yaliyo mbali ambapo mashambulizi mengi zaidi yanatokea na hayaripotiwi.

CHANZO:TRT Swahili