| Swahili
ULIMWENGU
2 dk kusoma
Mwanamke wa Kithailand akutwa hai ndani ya jeneza, mwili wake ukisubiriwa kuchomwa
Kulingana na msimamizi mkuu wa hekalu hilo, Pairat Soodthoop, mwili huo uliletwa na kaka wa marehemu hekaluni hapo, kwa ajili ya kuchomwa moto, kulingana na imani za Kibudha.
Mwanamke wa Kithailand akutwa hai ndani ya jeneza, mwili wake ukisubiriwa kuchomwa
Kulingana na ndugu wa marehemu huyo, mwanamke huyo alikuwa hajiwezi kitandani kwa kipindi cha miaka miwili./Picha:Reuters
24 Novemba 2025

Wafanyakazi wa hekalu moja nchini Thailand, walipigwa na butwaa baada ya mwili wa mwanamke uliokuwa ndani ya jeneza, kuanza kujisogeza.

Hekalu la mabudha la Wat Rat Prakhong Tham, lililoko kaskazini mwa Nonthaburi jijini Bangkok, liliweka picha mjongeo kwenye ukurasa wake wa Facebook, zikionesha mwili wa mwanamke uliowekwa kwenye sanduku jeupe, ukianza kujisogeza.

Kulingana na msimamizi mkuu wa hekalu hilo, Pairat Soodthoop, mwili huo uliletwa na kaka wa marehemu hekaluni hapo, kwa ajili ya kuchomwa moto, kulingana na imani za Kibudha.

Soodthoop alisema kuwa walishtushwa na sauti ya kugonga iliyokuwa inasikika kutoka ndani ya sanduku hilo, muda mfupi baada ya kuletwa hekaluni humo.

“Nilishtuka kidogo, nikasema wacha tulifungua jeneza hilo…tulistaajabu kuona marehemu huyo akifungua macho yake huku akiendelea kuligonga jeneza hilo,” alisema msimazi wa hekalu hilo.

Kulingana na ndugu wa marehemu huyo, mwanamke huyo alikuwa hajiwezi kitandani kwa kipindi cha miaka miwili, na afya yake kuzidi kudhoofika na hatimaye kuacha kupumua siku mbili zilizopita.

Hatua hiyo, ilimlazimu kaka wa marehemu huyo kuuweka mwili wake ndani ya jeneza na kuusafirisha kwa umbali wa kilomita 500, hadi kwenye hospitali moja mjini Bangkok, ili mwili huo uondolewe baadhi ya viungo vyake, kulingana na wosia wa mwanamke huyo.

Hata hivyo, hospitali hiyo ilikataa pendekezo hilo, ikisisitiza kuwa ilikuwa bado haijapokea cheti rasmi cha kifo cha mwanamke huyo.

Kulingana na Pirat, wakati wanajadili namna ya kupata cheti cha kifo cha mwanamke huyo ili waendelee na zoezi la kuuchoma mwili, ndipo waliposikia sauti ya kugonga kutoka ndani ya jeneza hilo.

Tayari, mwanamke huyo amepelekwa kwenye hospitali iliyo jirani kwa uchunguzi zaidi.

CHANZO:AP