| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Serikali ya Gabon yavunja timu ya taifa kufuatia matokeo ya AFCON
Serikali ya Gabon imetangaza kuiweka pembeni timu ya taifa ya soka kwa muda usiojulikana kufuatia matokeo mabaya kwenye michuano ya AFCON, ambapo ilipoteza mechi zote za hatua ya makundi.
Serikali ya Gabon yavunja timu ya taifa kufuatia matokeo ya AFCON
Timu ya Gabon ya iliomenyana na Côte d'Ivoire katika michuano ya AFCON. / / AP
1 Januari 2026

Serikali ya Gabon imetangaza kuvunjwa kwa timu ya taifa, kufukuzwa kwa kocha, na kutimuliwa kwa Pierre-Emerick Aubameyang kwenye kikosi kufuatia timu hiyo kupoteza mechi tatu katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).

Waziri wa Michezo wa Gabon alitangaza kupitia televisheni kuvunjwa kwa timu ya taifa baada ya kumaliza katika nafasi ya nne katika kundi lao na kuondolewa kwenye michuano hiyo yanayofanyika nchini Morocco.

“Kwa kuzingatia kiwango cha aibu kilichoonyeshwa na timu ya taifa kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika, serikali imeamua kuvunja benchi la ufundi, kuvunja timu ya taifa hadi itakapotangazwa vinginevyo, na kuwaondoa wachezaji Bruno Ecuele Manga na Pierre-Emerick Aubameyang,” alisema kaimu waziri wa michezo Simplice-Desire Mamboula baada ya kipigo cha 3–2 dhidi ya Côte d'Ivoire Jumatano huko Marrakech.

Gabon, iliyokuwa ikifundishwa na beki wa zamani Thierry Mouyouma, tayari ilikuwa imeshaondolewa baada ya kupoteza mechi zake mbili za kwanza za Kundi F dhidi ya Cameroon na Msumbiji.

Hata hivyo, katika mchezo wao wa mwisho walikuwa wanaongoza mabingwa watetezi kwa mabao 2–0 kabla ya kufungwa mabao matatu na kupoteza dhidi ya Côte d'Ivoire.

Kuumia kwa Aubameyang

Hata hivyo Aubameyang na beki mkongwe Ecuele Manga hawakushiriki katika mechi hiyo ya Jumatano, huku Aubameyang akirejea kwenye klabu yake ya Ufaransa, Olympique de Marseille, kwa matibabu ya jeraha la paja.

Mchezaji huyo aliyewahi kushinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika alijibu kupitia mitandao ya kijamii, wa X: “Nadhani matatizo ya timu ni makubwa zaidi kuliko mtu mmoja kama mimi.”

Aubameyang, mwenye umri wa miaka 36, huenda akawa amecheza mechi yake ya mwisho kwa Gabon katika mechi yao dhidi ya Msumbiji; naye piaEcuele Manga mwenye umri wa miaka 37, aliyewahi kuichezea Cardiff City, huenda akawa amecheza mechi yake ya mwisho.

Kuvunja au kusimamisha timu ya taifa ilikuwa hatua ya kawaida baada ya matokeo mabaya, lakini tangu shirikisho la soka duniani FIFA lichukue msimamo mkali dhidi ya kuingiliwa na serikali katika uendeshaji wa vyama vya soka, hatua hiyo imekuwa nadra sana kutokea.

Uamuzi wa kuvunjwa kwa timu umezua mjadala kuhusu nafasi ya serikali katika masuala ya soka.

CHANZO:AFP