Kuanguka kwa al-Fashir mnamo Oktoba 26 mikononi mwa RSF katika eneo zima la Darfur, kufuatia vita vilivyoendelea kwa zaidi ya miaka miwili na nusu dhidi ya jeshi la Sudan.
Wakimbizi kutoka mji huo wamesimulia jinsi raia walivyokuwa wakipigwa risasi na kushambuliwa kwa ndege zisizo na rubani.
Wanawake waliotoroka kutoka al-Fashir wamesema walishuhudia mauaji, ubakaji na watoto wao kupotea — “haya ni mateso ambayo hakuna mtu anayepaswa kuyapitia,” alisema Anna Mutavati, Mkurugenzi wa Kanda wa shirika la UN linaloshughulikia masuala ya wanawake kwa Afrika Mashariki na Kusini, alipohutubia waandishi wa habari mjini Geneva kupitia video kutoka Nairobi.
Mutavati alisema ukatili wa kijinsia umesambaa kwa kiwango kikubwa.
“Kuna ushahidi unaoongezeka kuwa ubakaji unatumika makusudi na kwa mpangilio kama silaha ya vita,” alisema.
“Miili ya wanawake imegeuzwa kuwa eneo la tukio la uhalifu nchini Sudan. Hakuna tena sehemu salama zilizobaki — hakuna mahali ambapo wanawake wanaweza kukusanyika kwa usalama, kutafuta hifadhi, au kupata hata huduma za kisaikolojia za msingi,” aliongeza.
Takriban wanawake na wasichana milioni 11 wanakabiliwa na ukosefu mkubwa wa chakula katika eneo la Darfur lililoathiriwa na njaa, na shirika la UN limeonya kwamba hata wanapojaribu kutafuta chakula, wanakabiliwa na hatari ya ubakaji na ukatili wa kijinsia.
Ripoti kutoka mashinani Darfur zinaeleza wanawake wakilazimika kutafuta majani pori na matunda ili kuchemsha na kutengeneza supu.
“Wanapofanya hivyo, wanajikuta wakikabiliwa na hatari zaidi za ukatili, ikiwemo utekaji na ukatili wa kijinsia,” alisema Mutavati.
Hivi karibuni, kikosi cha kimataifa cha ufuatiliaji wa chakula kilitangaza hali ya njaa katika al-Fashir na Kadugli, mji mwingine ulioko kusini mwa Sudan ambao pia uko chini ya mzingiro.
Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa alisema Ijumaa kuwa ana hofu mauaji ya kiholela, ubakaji, na mashambulizi yenye misingi ya kikabila yanaendelea katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, takriban watu 82,000 wamekimbia al-Fashir na maeneo ya jirani tangu Oktoba 26, huku inakadiriwa kuwa watu 200,000 bado wamekwama ndani ya mji huo kufikia mwisho wa miezi 18 wa kuzingirwa kwa mji huo.












