Novatus Miroshi Dismas amejiunga na mabingwa wa Ukraine Shakhtar kutoka Zulte Waregem ya Ubelgiji: Picha: Shakhtar Donetsk

Hatimaye baada ya kuwindwa na timu mbalimbali, nyota wa Taifa Stars Novatus Miroshi Dismas amesainiwa na Shakhtar Donetsk ya Ukraine ambapo ataihudumia kwa muda wa msimu mmoja wa 2023/24.

Beki huyo wa kushoto wa kimataifa raia wa Tanzania mwenye umri wa miaka 21, Miroshi, alikuwa akimezewa mate na timu za Middlesbrough na Southampton za Uingereza alipokuwa akiichezea klabu ya Zulte Waregem ya Ubelgiji.

Hata hivyo Shakhtar ilizipiku timu hizo na nyinginezo, na kumtia kapuni kutoka Zulte Waregem kwa njia ya mkopo kwani Novatus alisaini mkataba wa miaka mitatu na Zulte Waregem akishiriki mechi 38.

Miroshi alikuwa mvuto mkubwa akipiga ligi ya Tanzania akisakata Azam na Biashara United mbali na kuiwakilisha timu ya taifa ya Tanzania kwenye kombe la AFCON kwa Wachezaji chipukizi Afrika, nchini Mauritius.

Aidha, kiungo huyo wa kimataifa wa Tanzania alipiga jumla ya mechi 14 akiwa kikosini kwenye klabu hiyo kabla ya kuhamia timu ya daraja la pili ya Beitar Tel Aviv Bat Yam kwa njia ya mkopo kwa muda wa msimu mmoja wa msimu uliopita (2021/22).

Baada ya kuitumikia Beitar Tel Aviv Bat Yam kwa msimu mzima wa 2021/22, Novatus aliondoka kuelekea Ubelgiji baada ya Maccabi Tel Aviv FC kufikia makubaliano ya uuzaji wake kwa timu ya daraja la juu ya Ubelgiji S.V Zulte Waregem.

Mchezaji huyo, aliyetawazwa nyota wa chipukizi wa ligi ya Tanzania msimu uliopita wa 2019, Miroshi, alifuata nyayo za Mbwana Samatta na Kelvin John wa KRC Genk nchini Belgium na kuonyesha fomu ya juu zaidi.

Kwa upande wa timu ya taifa, Miroshi ni mchezaji wa kutegemewa na timu ya taifa ya Tanzania ambapo kufikia sasa amecheza zaidi ya mechi kumi tangu alipotinga uwanjani kwa mechi yake ya kwanza Septemba 2021.

Baada ya kukwea kutoka kituo cha ukuzaji vipaji cha Azam FC, sasa Mrisho anatarajiwa kuisaidia Shakhtar Donetsk ya Ukraine itakapokwatuana na miamba wa soka kwenye UEFA Champions League baadaye mwezi huu.

TRT Afrika