Uturuki inasherehekea kumbukumbu ya miaka 102 tangu kuanzishwa kwa Jamhuri ya nchi hiyo, huku Rais Erdogan akitoa wito wa umoja, uvumilivu, na kuendeleza maendeleo kuelekea dira ya taifa ya Karne ya Uturuki.
Kupitia ujumbe alioutoa Jumatano, Erdogan aliwapongeza wananchi wote wa Uturuki na wale wanaoishi nje ya nchi kwa Siku kuu ya Jamhuri, akiwatakia pia heri Waturuki wa Kupro na “marafiki wote wanaoshiriki furaha hii.”
“Katika siku hii ya fahari, nawapongeza kwa dhati raia wetu wote milioni 86, watu wa nchi ya Kupro ya Uturuki, na ndugu zetu wanaoishi nje ya nchi,” alisema. “Nawakumbuka na kuwaombea rehema ziwafikiw mashujaa walioufanya ardhi hii kuwa nchi yetu kwa kupitia damu na uhai wao.”
Erdogan alitoa heshima zake kwa mwanzilishi wa Jamhuri, Mustafa Kemal Ataturk, na Bunge Kuu la Kitaifa lililoongoza Vita vya Uhuru.
“Taifa lenye nguvu na mila zenye mizizi ya kihistoria”
Amesema Uturuki ni “taifa lenye nguvu na pia dola iliyo na mizizi ya kihistoria,” akisisitiza dhamira ya taifa hilo kulinda umoja na mamlaka yake.
Rais aliongeza kuwa Uturuki inaendelea kufanya “maboresho makubwa katika kila sekta” — kuanzia ulinzi, uchumi, nishati hadi diplomasia — chini ya dira ya Karne ya Uturuki, na akaahidi kuendelea kujenga “Uturuki kubwa, imara, na yenye ustawi.”
Erdogan pia aliahidi kuendeleza juhudi za kujenga upya maeneo yaliyoathiriwa na tetemeko la ardhi la Februari 2023, akibainisha kuwa serikali inalenga kukamilisha nyumba mpya 453,000 kufikia mwisho wa mwaka huu.
Alisisitiza tena dhamira ya Uturuki kwa amani na utulivu, akisema taifa hilo linaendelea “hatua kwa hatua kuelekea Uturuki isiyo na ugaidi,” huku likiendelea kutetea haki na ubinadamu katikati ya migogoro ya kimataifa, ikiwemo Gaza na Palestina.
“Pamoja, tutajenga Uturuki kubwa, imara, na yenye ustawi — kiongozi wa eneo letu na taifa linaloheshimiwa duniani,” Erdogan alisema alipoadhimisha kumbukumbu ya miaka 102 ya Jamhuri.

















