Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, amempokea Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, alipowasili katika Ikulu ya Rais jijini Ankara.
Erdogan na Starmer walipeana mikono na kupiga picha kwa ajili ya wanahabari wakiwa kwenye ngazi za ikulu, mbele ya bendera za Uturuki na Uingereza, siku ya Jumatatu.
Starmer aliambatana na Waziri wa Ulinzi wa Uingereza, John Healey, pamoja na Mkuu wa Majeshi ya Anga, Air Chief Marshal Harv Smyth.
Baada ya chakula cha jioni cha kikazi kati ya wajumbe wa pande zote mbili, viongozi hao watahudhuria hafla ya utiaji saini wa makubaliano na baadaye kufanya mkutano wa pamoja na wanahabari.
Miongoni mwa waliokuwepo katika hafla hiyo ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan, Waziri wa Ulinzi wa Kitaifa, Yasar Guler, Katibu Mkuu wa Ikulu, Hakki Susmaz, Balozi wa Uturuki nchini Uingereza, Osman Koray Ertas, Mkuu wa Mawasiliano, Burhanettin Duran, na Mshauri Mkuu wa Rais kuhusu Sera za Nje na Usalama, Akif Cagatay Kilic.
Katika ziara yake, Starmer anatarajiwa kumuarifu Erdogan kuhusu mazungumzo yanayoendelea kati ya Uturuki na Uingereza juu ya ununuzi wa ndege za kivita za Eurofighter Typhoon.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Burhanettin Duran kupitia jukwaa la kijamii la Uturuki, NSosyal, viongozi hao pia watajadili uhusiano wa mataifa mawili.
Duran aliongeza kuwa Rais Erdogan na Waziri Mkuu Starmer watazungumzia pia masuala ya sasa ya kikanda na ya kimataifa.
Awali, Starmer alitembelea Kiwanda cha Anga cha Uturuki (TUSAS) na kupewa maelezo kuhusu ndege ya kivita inayotengenzwa Uturuki inayojulikana kama KAAN, kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Uturuki.

















