Bunge la Libya limepinga matumizi ya nchi hiyo kuwa eneo la kufanyia operesheni za kijeshi zinazohusiana na migogoro ya mataifa ya nje, kufuatia mashambulizi yanayoshukiwa kufanywa kwa ndege zisizo na rubani dhidi ya meli mbili katika eneo la Benghazi.
Katika taarifa yake rasmi, Bunge la Wawakilishi la Libya lilisisitiza kuwa nchi hiyo haihusiki katika vita vinavyoendelea kati ya Urusi na Ukraine.
"Libya haihusiki katika vita vinavyoendelea kati ya Urusi na Ukraine," ilieleza taarifa ya bunge hilo.
Bunge hilo lilizitaka nchi za kikanda na jumuiya ya kimataifa kuheshimu mamlaka, uhuru na mipaka ya Libya. Pia lilionya mataifa ya kigeni dhidi ya kuchukua hatua zinazoweza kuivuta Libya katika migogoro ya kijeshi ya nje au kuhatarisha utulivu wa ndani wa nchi hiyo.
Aidha, bunge lilisisitiza kuwa uhusiano wa kidiplomasia au makubaliano yaliyopo kati ya Libya na mataifa mengine hayawezi kutumika kama sababu ya kuhalalisha mashambulizi dhidi ya miundombinu ya usalama wa nchi hiyo.
Libya yataka uchunguzi wa kimataifa
Bunge la Libya limesisitiza umuhimu wa kufanyika kwa uchunguzi ili kubaini waliohusika na mashambulizi hayo na kuhakikisha wanawajibishwa.
Pia lilieleza kuwa Libya ina haki ya kutumia njia za kisheria na kidiplomasia zinazotambuliwa na sheria za kimataifa ili kulinda maslahi na usalama wake.
Wabunge hao wamehuisha pia wito wa kuundwa kwa utawala mmoja wenye umoja nchini Libya, wakionya kuwa mgawanyiko wa kisiasa unaoendelea nchini humo unaifanya Libya kuwa katika hatari ya kuathiriwa na ushindani na migogoro ya mataifa ya nje.
Mashambulizi yaliyotokea siku ya Jumapili yalilenga meli ya Urusi iliyokuwa imetia nanga katika bandari ya Benghazi. Shambulizi hilo limewajeruhi wafanyakazi 10 wa bandari.
Meli nyingine iliyolengwa ilikuwa ya mizigo inayohusishwa na meli ya Malta. Baada ya tukio hilo, wafanyakazi wa meli hiyo waliondolewa kutoka kwenye meli hiyo kwa ajili ya usalama wao.
Mamlaka za mashariki mwa Libya zimethibitisha kuwasilisha malalamiko rasmi katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Kupitia malalamiko hayo, mamlaka hizo zimeomba uchunguzi wa kimataifa kuhusu mashambulizi hayo na pia zimetaka Ukraine itoe maelezo kuhusu shughuli zake za kijeshi nchini Libya.
Umoja wa Mataifa unataka uchunguzi huru
Kwa upande wake, Misheni ya Umoja wa Mataifa nchini Libya (UNSMIL) umeeleza wasiwasi mkubwa kuhusu kuongezeka kwa mashambulizi dhidi ya vyombo vya majini.
Katika taarifa iliyochapishwa siku ya Jumatatu kupitia mtandao wa X, ujumbe huo ulisema unaendelea kufuatilia kwa karibu hali inayoendelea.
UNSMIL imetoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi wa haraka, huru na ulio wazi kuhusu mashambulizi yaliyotokea katika bandari ya Benghazi na maeneo ya pwani ya Bahari ya Mediterania yanayoizunguka.













