Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewataka vijana kulinda amani na usalama wa nchi wakati taifa hilo linapojiandaa kuwa mwenyeji wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027.
Rais Samia ametoa wito huo Novemba 20, aliposimama Bomang’ombe, wilayani Hai, kwa ajili ya kuwasalimia wananchi wakati akiwa njiani kuelekea mjini Moshi.
“Ombi langu kwenu ni amani na utulivu kwa nchi yetu,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amesema matukio makubwa yanayoenda kufanyika nchini Tanzania ikiwemo AFCON 2027 na mashindano ya urembo wa dunia mwaka 2027 kuwa yanatarajiwa kuleta idadi kubwa ya wageni nchini humo.
Wakati huo huo, Rais Samia ametangaza Serikali kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa soko la kimataifa wilayani Hai.
“Ninataka niwahakikishie, tunakwenda kujenga soko la kimataifa ndani ya wilaya hii,” amesema Rais Samia, na kuongeza kuwa soko hilo litawapa wakulima sehemu ya uhakika ya kuuza mazao yao.














