Rais wa Kenya, William Ruto, amewasili mjini Oyo, Jamhuri ya Congo, kushiriki Mkutano wa Nchi Nne unaowakutanisha viongozi kutoka Jamhuri ya Congo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Togo na Kenya.
Kupitia ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa X, Ruto amesema mkutano huo utajadili masuala muhimu yanayolenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, kuongeza ushirikiano wa kikanda, kuendeleza amani na usalama, pamoja na kupanua ushirikiano kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa pamoja wa mataifa hayo.
Aidha, Rais Ruto amesisitiza umuhimu wa mazungumzo, ushirikiano na kutafuta suluhisho linaloongozwa na Waafrika wenyewe katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili Afrika.
Mkutano huo unatajwa kuwa sehemu ya juhudi za kuimarisha mshikamano wa mataifa ya Afrika na kukuza ushirikiano katika masuala ya kisiasa, kiusalama na kiuchumi kwa manufaa ya wananchi wake.














