Umoja wa Afrika umelikosoa vikali shambulio la hivi karibuni lililosababisha vifo kaskazini-magharibi mwa Nigeria, na kuelezea mashambulizi katika Jimbo la Zamfara kama "tendo la kigaidi na kikatili" hivyo kuhimiza hatua za pamoja za mamlaka ili kulinda wakazi wa maeneo hayo.
Katika taarifa iliyotolewa kwa niaba ya taasisi hiyo, Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Mahmoud Ali Youssouf, alikemea vikali mashambulizi ya Februari 21, 2026 katika Jimbo la Zamfara yaliyosababisha vifo vya zaidi ya raia 50 na kutekwa kwa wanawake na watoto kadhaa.
"AU inatoa wito wa kuachiliwa mara moja kwa wanawake wote na watoto waliotekwa, wakiwa salama, na bila masharti," ilisema taarifa.
Kulingana na maafisa wa eneo hilo, wanamgambo waliingia katika kijiji cha Tungan Dutse katika Eneo la Serikali ya Mitaa la Bukkuyum Alhamisi jioni, na kuwashambulia wakazi kuanzia saa kumi na moja jioni.
Kuongezeka kwa changamoto za usalama
Kaskazini-magharibi imekuwa ikikabiliwa kwa miaka mingi na wimbi la uhalifu wa wanamgambo, utekaji wa watu kwa kwa lengo la kudai fidia, na mashambulizi ya vijijini, wakati sehemu nyingine za nchi zinakabiliana na uasi katika kaskazini-mashariki.
Pia kuna mvutano wa kutaka kujitenga katika eneo la kusini-mashariki na mgongano wa kijamii katika maeneo ya katikati ya nchi.
Wavamizi wa Zamfara walichoma nyumba na kuwasha moto dhidi ya wakazi waliokuwa wanajaribu kukimbia.
Hamisu A. Faru, mbunge anayewakilisha Bukkuyum Kusini, aliiambia Reuters kwamba takriban watu 50 waliuawa.
Umoja wa Afrika umesema kwamba unalaani vikali vitendo vyote vya ugaidi dhidi ya wakazi, hasa wanawake na watoto, na kuyaelezea mauaji na utekaji kama ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.
Youssouf alielezea mshikamano kamili wa Umoja wa Afrika na serikali na wananchi wa Nigeria, huku akituma salamu zake za rambirambi kwa familia zilizoachwa na wafiwa na kuwatakia uponyaji wa haraka waliojeruhiwa.
Licha ya kuongezeka kwa oparesheni za kijeshi na ahadi za serikali kurejesha utulivu, jamii za vijijini katika majimbo kama Zamfara, Kaduna, na Katsina zinaendelea kuwa hatarini kutokana na makundi yenye silaha nzito.
Wabunge na mashirika ya kiraia wamekuwa wakitaka ukusanyaji bora wa taarifa za kijasusi na ulinzi wa kina kwa jamii za pembezoni.















