Khalid Aucho: Nahodha wa timu ya Uganda
Khalid Aucho, kiungo wa Singida Big Stars ya Tanzania.
Khalid Aucho: Nahodha wa timu ya Uganda
Nahodha wa timu ya taifa ya Uganda ni Khalid Aucho ambaye kwa sasa anakipiga na timu ya katikati mwa Tanzania Singida Black Stars.
5 Desemba 2025

Mchezaji huyu kiungo mkabaji anajulikana kama ‘‘Dokta’’ kutokana na utaalamu wake uwanjani.

‘‘Dokta’’ Aucho amewahi kucheza katika timu nyingi ikiwemo Water FC ya Uganda, Simba ya Uganda, Tusker FC na Gor Mahia za Kenya na Baroka ya Afrika Kusini.

Kama ulikuwa hufahamu Khalid Aucho amecheza katika Ligi zingine ambazo pengine hujawahi kuzisikia. Fundi huyu mwenye umri wa miaka 32 amecheza katika ligi ya Serbia na timu ya ligi daraja la pili ya Misri ya Misr lel-Makkasa.

Pengine mmezoea India kuna sinema za Bollywood au kriketi, Dokta Aucho alicheza pia huko akiwa na timu za East Bengal na Churchill Brothers.

Lakini ni wazi nyota yake iling’aa zaidi alipojiunga na Wananchi, mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania, Young Africans mwaka 2021.

Amekuwepo Jangwani kwa misimu minne tangu alipojiunga nao msimu wa kwanza 2021/22.  Aliipatia timu hiyo magoli mawili.

Kiungo mkabaji huyo alianza kucheza katika timu ya taifa ya Uganda mwaka 2013 na amekuwa sehemu muhimu wa timu hiyo ya the Cranes hadi leo ambapo ni nahodha wa timu hiyo.

Alikuwa miongoni mwa kikosi kilichoipeleka timu hiyo ya ardhi ya matoke kwenye fainali za kombe la mataifa ya Afrika mwaka 2016 baada ya miaka 38.

Amecheza pia kwenye mashindano ya CECAFA na michezo mingine. Kwa sasa Dokta Aucho anapambania kuhakikisha Singida Big Stars inabaki kuwa kubwa kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

 

CHANZO:TRT Afrika Swahili