AFRIKA
1 dk kusoma
‘Karibuni Tanzania, ipo salama’, yasema Wizara ya Utalii
Hakikisho hilo linafuatia vurugu zilizoibuka wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 na kusabisha vifo vya watu, majeruhi na uharibu wa mali.
‘Karibuni Tanzania, ipo salama’, yasema Wizara ya Utalii
Tanzania inasifika ulimwenguni kwa utajiri wake wa maliasili./Picha:Getty
tokea masaa 3

Wizara ya Maliasili na Utalii ya Tanzania imeuhakikishia umma wa Watanzania, wageni kutoka nje na wadau wengine wa utalii, kuhusu usalama wa nchi hiyo.

Katika taarifa yake ya Novemba 4, 2025, Wizara hiyo imesema kuwa hali ya amani na utulivu, imerejea nchini humo huku shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi zikiendelea baada ya kudhibitiwa ka vurugu zilizoibuka kati ya Oktoba 29 na Novemba 1, 2025.

“Tanzania kama mwanachama wa Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism), inatekeleza na kusimamia Mwongozo wa Utalii Kimataifa unaoelekeza nchi kuhakikisha usalama wa wageni, ikiwemo wasafiri na watalii wanaotembelea maeneo mbalimbali wawapo nchini,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Kulingana na Wizara hiyo, vituo vyote vya kuingia na kutokea nchini humo kupitia usafiri wa anga, barabara, maji, reli na usafiri wa umma, vinaendelea kutoa huduma kwa utaratibu wa kawaida.

Aidha, shughuli za utalii na huduma kwa wageni zinaendelea kutolewa katika maeneo yote nchini humo kushirikiana na sekta binafsi.

“Wasafiri wanahimizwa kuendelea na mipango yao ya kutembelea na kufurahia vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo Tanzania bila hofu yoyote,” taarifa hiyo ilisema.

Hakikisho hilo linafuatia vurugu zilizoibuka wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 na kusabisha vifo vya watu, majeruhi na uharibu wa mali.