Manchester United imegeuka kama kituo cha majaribio ya makocha! Tangu Sir Alex Ferguson aondoke mwaka 2013, klabu hiyo haijashinda tena taji la Premier League, licha ya kumwaga mabilioni ya fedha na kuajiri makocha kadhaa wakubwa.
Sasa Michael Carrick ameshindwa kuendelea na kazi yake. Nafasi yake inachukuliwa na Mauricio Pochettino.
Lakini tatizo la United ni nini hasa?
Carrick ameondoka baada ya kuanza vibaya msimu wa 2026/27. Ushindi mmoja tu katika mechi kumi za ligi, pointi nane na timu kujikuta kwenye eneo la kushuka daraja. Kwa matokeo hayo, ilikuwa vigumu kuendelea kumvumilia.
Lakini je, lawama zote ni zake?
United imetumia pauni milioni 163 kwenye usajili wa majira ya kiangazi, lakini bado ina mapengo kwenye safu ya ulinzi na ushambuliaji. Hapo ndipo maswali yanapoanzia: Nani anapanga usajili? Nani anaamua mwelekeo wa timu? Na mambo yanapoharibika, nani anawajibika?
Pochettino anakuja na uzoefu wa Premier League na falsafa ya soka la kushambulia. Lakini atapewa uhuru na sapoti ya kujenga timu anayoitaka?
Jaribio lake la kwanza ni Jumapili hii, Anfield dhidi ya Liverpool. Je, ataanza kwa kishindo au atakutana na yale yale yaliyomponza Carrick?
Huenda Carrick ana sehemu ya lawama, lakini haiwezekani matatizo yote ya United yakawa ya makocha pekee.
Swali la msingi si nani anakaa kwenye benchi la United, bali ni nani anayeisimamia klabu hii na kwa mipango gani?
MICHEZO
2 dk kusoma
Manchester United: Je, Pochettino ndiye dawa au tatizo ni klabu yenyewe?
Pochettino anakuja na uzoefu wa Premier League na falsafa ya soka la kushambulia. Lakini atapewa uhuru na sapoti ya kujenga timu anayoitaka?

Soma zaidi













