Chuo Kikuu cha Kordofan nchini Sudan kimesema kuwa ndaki yake katika mji wa El-Obeid imepata uharibifu mkubwa baada ya ndege zisizo na rubani ambazo imesema zinamilikiwa na RSF kushambulia eneo la chuo Jumatatu.
Katika taarifa yake, ofisi ya waandishi wa habari ya Chuo Kikuu imesema shambulio hilo limelenga majengo katikati ya ndaki ya El-Obeid, katika mji mkuu wa Kaskazini mwa Jimbo la Kordofan, na kusababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu.
Hakuna taarifa zaidi kuhusu waliojeruhiwa.
Muungano wa Mawakili wa Dharura, makundi ya kutetea haki za binadamu, wamelaani shambulio hilo na kutaka RSF kuwajibishwa, na kulielezea tukio hilo kama muendelezo wa mashambulizi dhidi ya maeneo ya raia.
Kushambulia taasisi za elimu ni "ukiukaji wa sheria za kimataifa," lilisema kundi hilo, na kusisitiza kuwa mashambulizi katika vyuo vikuu ni kikwazo cha upatikanaji wa elimu hivyo kuhatarisha mustakbali wa wanafunzi.
Sudan imekuwa katika vita kati vya jeshi na vikosi vya RSF tangu Aprili 2023, na kusababisha vifo vya maelfu ya watu, huku takriban watu milioni 13 wakikosa makazi, na kusababisha moja ya majanga makubwa ya kibinadamu, kwa mujibu wa ripoti ya UN.














