Rais wa Sierra Leone: Julius Maada Bio
Rais wa Sierra Leone Julius Maada Bio. / Reuters
Rais wa Sierra Leone: Julius Maada Bio
Unafahamu taifa la Sierra Leone lenye idadi ya watu milioni 9? Nchi hiyo iko Afrika Magharibi na Rais wake ni Julius Maada Bio.
26 Novemba 2025

Kiongozi huyo wa sasa amekuwa madarakani tangu mwaka 2018, alipigiwa kura kwa muhula wa pili mwaka 2023. Muhula wa Urais ni miaka mitano na katiba inaruhusu mihula miwili tu.

Julius Maada Wonie Bio ni rais wa awamu ya tano wa taifa hilo na ni Brigedia mstaafu wa jeshi la Sierra Leone au kama wenyewe wanavyolitambua Salone.

Aliwahi kuwa kiongozi wa kijeshi wa nchi hiyo kwa miezi takriban mitatu akiwa na umri wa miaka 32 tu mwaka 1996

Anatambulika kwa kurejesha uongozi kwa serikali iliyokuwa imechaguliwa kwa njia ya demokrasia ya Ahmad Tejan Kabbah.

Baada ya hapo alielekea Marekani alipopata hifadhi ya kisiasa na kurudi tena Sierra Leone mwaka 2005.

Maada Bio aligombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2012 lakini akashindwa na kiongozi aliyekuwepo madarakani wakati huo Ernest Bai Koroma.

Akarudi tena uwanjani 2018 na kufanikiwa kumshinda mgombea wa chama tawala Samura Kamara., katika duru ya pili. Mwaka 2023 kulikuwa na jaribio na kupindua serikali ya Maada Bio.

Katika tukio hilo mtangulizi wake Ernest Bai Koroma alikamatwa na kushtakiwa kwa uhaini akishtumiwa kuhusika na jaribio la mapinduzi.

Kwenye uchaguzi wa 2023 Julius Maada Bio alichaguliwa mitano tena katika nchi hiyo iliyo ya saba kwa utajiri wa almasi barani Afrika.

Alizaliwa miaka 61 iliyopita katika kijiji cha Tihun, mkoa wa kusini nchini Sierra Leone. Wakati nchi hiyo ikipata uhuru, Bio alikuwa na umri wa miaka mitatu tu mwaka 1961.

Yeye mwenyewe ni mtoto wa 33 kati ya 35 wa Chifu Charlie Bio wa pili wa jamii ya Sherbro, ukoo wa Sogbini. Baba yake alikuwa na wake tisa.

Makamu wake wa rais ni Mohamed Juldeh Jalloh na serikali yake itamaliza muhula wa pili na wa mwisho mwaka 2028.

CHANZO:TRT Afrika Swahili