Shirika la Ndege la Uturuki limeanza tena safari za moja kwa moja kuelekea Sudan baada ya kusitisha huduma kwa miezi 29 kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Sudan imekuwa ikikumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya jeshi la taifa na kikosi cha wanamgambo cha Rapid Support Forces (RSF) tangu Aprili 2023, hali ambayo imesababisha vifo vya maelfu ya watu na mamilioni kuyahama makazi yao, kulingana na mashirika ya Umoja wa Mataifa.
Balozi wa Uturuki nchini Sudan alitangaza kurejea kwa safari za shirika hilo kuelekea Port Sudan, mji mkubwa zaidi wa bandari nchini humo.
"Kwa safari hizi, Waturuki na Uturuki kwa mara nyingine wameonyesha mshikamano wao na marafiki zao katika nyakati ngumu," alisema Balozi Fatih Yildiz.
‘Kuonyesha urafiki’
"Kupitia safari hizi, tumetoa ujumbe mzito kwamba Sudan haiko peke yake, kwamba tumejizatiti kupinga wale wanaotaka kuitenga Sudan, na kwamba tumeonyesha urafiki wetu," alisema.
"Safari hizi zinaonyesha kuwa Shirika la Ndege la Uturuki ni nguzo muhimu ya sera ya kigeni na diplomasia ya Uturuki," aliongeza.
Kwa kuanzisha safari za kuelekea Port Sudan, Turkish Airlines sasa imeongeza idadi ya maeneo inayoenda barani Afrika kufikia 63.