Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zimetia saini makubaliano ya amani nchini Marekani, yenye lengo la kumaliza mgogoro uliopo nchini DRC. Mkataba huu uliosimamiwa na Marekani, unataka nchi husika kuheshimiana, kupokonywa silaha kwa makundi yasiyo ya serikali, na kuwepo kwa utaratibu wa pamoja wa kuratibu usalama.
Hata hivyo, ni wazi kwamba aliyefaidika zaidi katika makubaliano hayo ni Marekani, ambayo kupitia usimamizi wa mchakato huyo, tayari imeingia makubaliano ya kupata madini kutoka nchi hizo mbili.
"Na tutatuma baadhi ya makampuni yetu makubwa zaidi ya Marekani kwa nchi hizi mbili," Trump alisema.
Mnamo Machi 2025, ilibainika kuwa Rais wa DRC Felix Tshisekedi alipendekeza kwa Marekani kuwezesha upatikanaji wa madini ya kimkakati - kama vile coltan na dhahabu - muhimu kwa sekta ya teknolojia, ili kubadilishana na makubaliano rasmi ya usalama ili kukabiliana na M23.
Mara tu baada ya mkataba wa DRC na Rwanda kusainiwa Marekani na DRC sasa zimesaini mkataba wa uhusiano wa kimkakati kati yake na DRC.
Mkataba mpya kati ya Marekani na DRC
"Tunasuluhisha vita ambavyo vimekuwa vikiendelea kwa miongo kadhaa," Trump alisema.
"Walitumia muda mwingi kuuana, na sasa watatumia muda mwingi kukumbatiana, kushikana mikono, na kutumia fursa ya Marekani kiuchumi - kama kila nchi nyingine."
Na mkataba huu unahusisha kuipa Marekani kipaumbele katika kufua madini nchini DRC. DRC ina akiba nyingi za kobalti, koltani, shaba, dhahabu na lithiamu ambazo hazijatumika, madini muhimu katika sekta ya nishati duniani.
Trump alifanya mikutano tofauti na viongozi hao wawili wa Kiafrika katika Ikulu ya White House siku ya Alhamisi asubuhi.
Mwezi Juni 2025, mapatano ya awali ya amani yalitiwa saini na mawaziri wa Mambo ya Nje wa DRC na Rwanda mjini Washington.
Kumuondoa China katika biashara wa madini
Chini ya mkataba mpya na Marekani, DRC sasa inatakiwa kutoa orodha ya awali ya rasilimali muhimu za madini, na maeneo ambayo hayana leseni kama sehemu ya Hifadhi yake Mali ya Kimkakati. Itatakiwa kutoa orodha hii ndani ya siku thelathini (30) baada ya kuanza kutumika kwa Makubaliano haya.
Wakati wowote, rasilimali muhimu za ziada za madini, rasilimali za dhahabu, na maeneo yasiyo na leseni yanaweza kuongezwa na DRC kwenye orodha hii. Na udhibiti wa maelezo haya yatakuwa chini ya kamati ya pamoja itakayoundwa kati ya Marekani na DRC.
“Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inajitolea kutekeleza, kwa dhati kabisa, majukumu yote yanayotokana na Makubaliano haya,” Felix tshisekedi, Rais wa DRC alisema.
“Tutafanya hivyo kwa umakini, kwa ukali, na kwa kujali mara kwa mara amani, usalama wa watu wetu.”
Lakini wataalamu wanasema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa Marekani wa kupunguza utegemezi kwa China, ambayo kwa sasa inadhibiti zaidi ya 70% ya uchimbaji madini adimu duniani na zaidi ya 85% ya usindikaji.
Nchini DRC, China imekuwa ikifua madini, hasa kobalti tangu mwaka 2008, ilipofanya makubaliano na serikali ya DRC yaliyoitwa mkataba wa Sino Congolaise des Mines (Sicomines).
Walakini, mikataba hii ni ya masharti.
Ushirikiano wa kiuchumi utaanzishwa kikamilifu ikiwa tu usitishaji wa mapigano utaendelea na uondoaji wa kijeshi utaheshimiwa.
Na huku Marekani ikijitayarisha kupelekea makampuni yake makubwa kufua madini nchini DRC, maelfu ya watu wanaoteseka kutokana na kutokuwepo na usalaama nchini DRC, wamebaki bila kuelewa makubaliano haya mapya ya Washington yatarudisha vipi hali ya usalama na utulivu maishani.










