| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Baadhi ya nchi za Magharibi zataka Tanzania ikabidhi maiti za waliouawa baada ya uchaguzi
Balozi kadhaa zilizopo nchini Tanzania ikiwemo ile ya Uingereza, Canada, Norway, Uswizi, Denmark na jopo la Umoja wa Ulaya, zimetoa wito kwa serikali ya Tanzania kukabidhi maiti kwa ndugu zao na kuwaachia wafungwa wa kisiasa.
Baadhi ya nchi za Magharibi zataka Tanzania ikabidhi maiti za waliouawa baada ya uchaguzi
Rais Samia ameunda Tume maalumu ambayo imepewa jukumu la kuchunguza vurugu za Oktoba 29./ / Reuters
tokea masaa 2

Serikali ya Tanzania imetakiwa kukabidhi miili ya waliouawa baada ya uchaguzi mkuu kwa ndugu zao, pamoja na kuwaachia wafungwa wote wa kisiasa.

Kauli hii imetolewa kwa pamoja na balozi kadhaa zilizopo nchini Tanzania ikiwemo ile ya Uingereza, Canada, Norway, Uswizi, Denmark na jopo la Umoja wa Ulaya.

Kauli hii inakuja kufuatia vurugu zilizotokea nchini humo baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, ambapo taarifa hiyo imesema kuwa, kuna ushahidi wa kutosha kutoka mashirika ya kimataifa na ya ndani unaoonesha kufanyika kwa mauaji, watu kupotea na wengine kukamatwa.

"Ripoti za kuaminika kutoka mashirika ya ndani na kimataifa zinaonyesha ushahidi wa mauaji, kupotea kwa watu na wengine kukamatwa," limesema tamko hilo la pamoja, na kuitaka serikali ya Tanzania kufuata mapendekezo yaliyotolewa na AU na SADC kuhusu mapungufu yaliyojitokeza wakati wa Uchaguzi Mkuu.

Kufuatia Uchaguzi  Mkuu nchini Tanzania ambao matokeo yake yalimtangaza Rais Samia Suluhu Hassan kwa ushindi wa asilimia 98, nchi hiyo ya Afrika Mashariki, imekuwa ikimulikwa kutokana na vurugu zilizoibuka baada ya Uchaguzi, ambapo mbali na mauaji yaliyotokea, lakini pia kumekuwa na uharibifu mkubwa wa mali za watu binafsi na serikali.

Hata hivyo, serikali ya nchi imehusisha vurugu hizo na makundi ya uhalifu. Wakati huo huo, Rais Samia ameunda Tume maalumu ambayo imepewa jukumu la kuchunguza vurugu za Oktoba 29 na kuweka wazi ripoti. Tume hiyo inaongozwa na Jaji Mkuu mstaafu wa Tanzania Mohamed Chande.

Haya yanajiri wakati kukiwa taarifa za kuwepo kwa maandamano Disemba 9, maandamano yanayoratibiwa kupitia mitandao ya kijamii lenye lengo la kuishinikiza serikali kufanya mabadiliko kadhaa ikiwemo ya katiba.

Kwa upande wake, polisi nchini humo imewatahadharisha watakaoshiriki maandamano hayo na kusema sio halali. Tayari hofu imetanda katika jamii, huku baadhi wakianza kununua vyakula na kuweka ndani kama sehemu ya tahadhari ya siku hiyo.

CHANZO:TRT Afrika