| Swahili
ULIMWENGU
3 dk kusoma
Trump atishia shambulio la pili Venezuela, aonya kuhusu operesheni nyingine Colombia
Rais wa Marekani Donald Trump amesema operesheni ya kijeshi nchini Colombia “inaonekana kuwa wazo zuri,” akidai kuwa nchi hiyo inaendeshwa na “mtu mgonjwa.”
Trump atishia shambulio la pili Venezuela, aonya kuhusu operesheni nyingine Colombia
Trump anazungumza na waandishi wa habari akiwa ndani ya ndege ya Air Force One akitokea Florida kuelekea Joint Base Andrews. / / Reuters
5 Januari 2026

Rais Trump ametishia kuishambulia Venezuela kwa mara ya pili iwapo “hawatobadilisha mwenendo,” huku pia akitishia kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya serikali ya Colombia.

Akizungumza na waandishi wa habari, alisema kuwa operesheni kama hiyo “inaonekana kuwa wazo zuri kwake.”

“Tunakabiliana na watu ambao ndiyo kwanza wameapishwa madarakani. Msiniulize ni nani aliye madarakani kwa sababu nitatoa jibu litakalokuwa na utata mkubwa,” Trump aliwaambia waandishi wa habari akiwa ndani ya ndege ya Air Force One, alipoulizwa kama amezungumza na kiongozi wa mpito Delcy Rodriguez.

Aliposisitizwa kueleza alichomaanisha, Trump alisema: “Hii ina maana kwamba sisi ndiyo tuko madarakani.”

Wakati huo huo, Delcy Rodriguez siku ya Jumapili alitoa wito wa kuwepo kwa uhusiano wa “usawa na wa heshima” kati ya Venezuela na Marekani, siku moja baada ya majeshi ya Marekani kuishambulia Caracas na kumkamata kiongozi wa mrengo wa kushoto, Nicolas Maduro.

“Tunaona kuwa ni kipaumbele kusonga mbele kuelekea uhusiano wa usawa na wa heshima kati ya Marekani na Venezuela,” Rodriguez, ambaye ni makamu wa rais wa Maduro, aliandika kwenye Telegram.

“Tunaialika serikali ya Marekani kushirikiana nasi katika ajenda ya ushirikiano inayolenga maendeleo ya pamoja.”

Trump: Operesheni nchini Colombia “inaonekana kuwa wazo zuri”

 Akizungumzia Colombia, Trump alisema nchi hiyo inaendeshwa na “mtu mgonjwa,” na akasema operesheni ya kijeshi huko “inaonekana kuwa wazo zuri.”

“Colombia nayo ina matatizo, inaendeshwa na mtu mgonjwa, anayependa kutengeneza kokeini na kuiuza Marekani, na hataendelea kufanya hivyo kwa muda mrefu,” Trump aliwaambia waandishi wa habari, akionekana kumuashiria Rais wa Colombia, Gustavo Petro.

Alipoulizwa moja kwa moja kama Marekani ingefanya operesheni ya kijeshi dhidi ya Colombia, Trump alijibu: “Inaonekana kuwa wazo zuri kwangu.”

Kauli hizo zilitolewa baada ya Marekani kumteka nyara Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro, katika oparesheni ya kushtukiza na kumpeleka New York ili akabiliane na mashtaka ya biashara ya dawa za kulevya.

Cuba “iko karibu kuanguka”

Trump pia alizungumzia Cuba, akisema kuwa nchi hiyo “iko tayari kuanguka” baada ya majeshi ya Marekani kumkamata kiongozi wa mshirika wake, wa Venezuela, huku akipunguza haja ya hatua za kijeshi za Marekani dhidi ya Cuba.

“Cuba iko tayari kuanguka,” Trump aliwaambia waandishi wa habari, akisema itakuwa vigumu kwa Havana “kuhimili” bila kupata mafuta ya bei nafuu kutoka Venezuela.

“Sidhani kama tunahitaji kuchukua hatua yoyote. Inaonekana mambo yanaelekea kuanguka yenyewe.”

Wakati huo huo, serikali ya Cuba ilisema jumla ya raia 32 wa Cuba waliuawa katika shambulio la Marekani mjini Caracas.

“Kutokana na shambulio la kinyama lililofanywa na serikali ya Marekani dhidi ya Venezuela, Wacuba 32 walipoteza maisha yao katika operesheni za mapigano,” serikali ya Cuba ilisema katika taarifa iliyosomwa kwenye runinga ya taifa.

 

 

 

 

CHANZO:TRT World and Agencies