Maelfu ya Watanzania wanaotegemea sekta ya madini kama chanzo kikuu cha mapato wanatarajiwa kuanza kunufaika zaidi baada ya Serikali kuanza utekelezaji rasmi wa Kanuni ya 13, inayolenga kuwalinda wazawa katika sekta hiyo.
Serikali imetangaza kufanya marekebisho ya Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania za mwaka 2018, ambapo kupitia Kanuni ya 13A, Tume ya Madini itakuwa ikitangaza mara kwa mara orodha ya bidhaa na huduma zinazopaswa kutolewa na kampuni zinazomilikiwa kwa asilimia 100 na Watanzania.
Lengo ni kupanua wigo wa ushiriki wa wazawa na kuongeza manufaa ya moja kwa moja kwa taifa.
Hatua hiyo inatarajiwa kupunguza malalamiko ya muda mrefu kwamba rasilimali za madini haziwanufaishi Watanzania ipasavyo. Marufuku hiyo, iliyoanza kutekelezwa Novemba 15 mwaka jana, imetangazwa rasmi leo na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde.
Akizungumza na vyombo vya habari Jijini Dodoma, Mavunde amesema miongoni mwa maeneo yaliyopigwa marufuku kwa wageni ni uchimbaji wa moja kwa moja, ambapo sasa utaruhusiwa tu kwa mfumo wa mkataba, pamoja na usambazaji wa jumla wa vilainishi na mafuta ya kulainisha mitambo.
“Migodi mikubwa imekuwa ikiagiza bidhaa kutoka nje, hata zile zinazopatikana nchini, hali iliyosababisha fedha nyingi kutoka nje ya nchi bila kuzinufaisha Serikali,” alisema Mavunde, akiongeza kuwa hata bidhaa za msingi kama mayai na kuku ziliwahi kuagizwa kutoka nje.
Kwa mujibu wa Serikali ya Tanzania, utekelezaji wa kanuni hizo unalenga kuongeza ajira, kukuza nafasi za uongozi kwa wazawa na kuimarisha mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa taifa.
Katika miaka ya hivi karibuni, Tanzania imechukua hatua kadhaa za kuimarisha sekta hiyo, ikiwemo ujenzi wa viwanda vya kuchakata madini, maabara, pamoja na marekebisho ya baadhi ya sheria zilizokuwa zikionekana kuwa kandamizi kwa wazawa.
Hata hivyo, Serikali inakiri kuwa changamoto kubwa imekuwa kwenye utekelezaji wa sheria hizo.
Wizara ya Madini sasa imetunga kanuni mpya zinazoweka zuio kwa zaidi ya bidhaa 20 kufanywa na wageni, hatua inayolenga kuhakikisha Watanzania wanapata manufaa halisi ya rasilimali za madini zilizopo nchini.




















