Kampeni za uchaguzi wa urais wa mwezi ujao katika Jamhuri ya Congo zinaanza Jumamosi, na Rais Denis Sassou Nguesso, mwenye umri wa miaka 82, ndiye mgombea anayepigiwa upatu kushinda.
Afisa huyo wa kijeshi aliongoza Jamhuri ya Congo, ambayo pia inajulikana kama Congo-Brazzaville, chini ya mfumo wa chama kimoja kutoka 1979 hadi 1992, kabla ya kushindwa katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi nchini humo kwa waziri mkuu wa zamani Pascal Lissouba.
Alimpindua Lissouba katika vita vya wenyewe kwa wenyewe ili kurejea madarakani mwaka 1997.
Mapema mwezi huu, alitangaza kuwa atawania muhula mpya wa miaka mitano, ambao, kwa mujibu wa katiba, ungekuwa mwisho wake.
Kampeni zinaanza Jumamosi kwenye pwani ya Atlantiki katika mji mkuu wa uchumi na mafuta wa nchi hiyo, Pointe-Noire, kwa mkutano unaofanywa na chama cha rais cha Congolese Labour Party (PCT).
Itakamilika Machi 13, na duru ya kwanza ya upigaji kura mnamo Machi 15.
Wagombea sita wa upinzani wametangaza rasmi kushiriki, ikiwa ni pamoja na Destin Gavin mwenye umri wa miaka 34, kutoka chama cha Harakati ya Republicani (MR), ambaye anagombea kwa mara ya kwanza.
Lakini upinzani uliogawanyika hauko na nafasi kubwa ya kushinda, huku chama tawala kikiahidi 'kufagia kura ' kwa mzee wa taifa', kulingana na mabango ya kampeni kando ya barabara.
Sassou Nguesso ni mmoja wa viongozi waliodumu madarakani kwa muda mrefu barani Afrika, baada ya Paul Biya wa Cameroon, ambaye yuko madarakani tangu 1982, na Teodoro Obiang Nguema Mbasogo wa Guinea Ikweta, aliyechukua madaraka kwa mapinduzi mwaka 1979.









