Hebu fikiria umefika umri wa miaka 70 au 80 baada ya muda mrefu wa kufanya kazi, kulea familia na kuchangia katika jamii, lakini unajikuta ukinyanyaswa na watu unaowaamini zaidi katika maisha yako.
Inaonekana jambo lisilowezekana, lakini kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), unyanyasaji kwa wazee umekuwa mojawapo ya majanga ya afya ya umma yanayokua kwa kasi zaidi duniani huku yakijadiliwa kwa uchache.
Na kadiri watu wanavyozeeka, WHO inaonya kuwa tatizo hili litazidi kuwa baya zaidi.
Unyanyasaji kwa wazee ni nini ?
WHO inafafanua kuwa, unyanyasaji kwa wazee ni kitendo chochote au hali ya kushindwa kuchukua hatua ya kuwatetea, ndani ya uhusiano unaotegemea kuaminiana, ambao husababisha madhara au dhiki kwa mtu mwenye umri wa miaka 60 na zaidi.
Unyanyasaji huo sio lazima uwe wa kimwili pekee. Unaweza kuwa wa kihisia, kisaikolojia, kiuchumi au kingono.
Unaweza pia kujitokeza kwa njia ya kutelekezwa, ambapo wazee hunyimwa chakula, dawa, huduma au hata heshima ya msingi anayostahili kupewa binadamu.
Takwimu za kutisha
Ukubwa wa tatizo hili ni wa kutisha. Kulingana na WHO, takriban mtu mmoja kati ya sita wenye umri wa miaka 60 na zaidi amekumbana na aina fulani ya unyanyasaji katika jamii zao katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Hiyo ni karibu na asilimia 16 ya idadi ya wazee duniani.
Hali ni mbaya zaidi ndani ya vituo vya kuwatunza wazee. Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema karibu wafanyakazi wawili kati ya watatu katika nyumba za wazee na vituo vya kutunza wazee kwa muda mrefu walikiri kufanya aina fulani ya unyanyasaji katika mwaka uliopita.
Watafiti pia waligundua kuwa unyanyasaji uliongezeka wakati wa janga la COVID-19. Utafiti mmoja nchini Marekani ulionesha kuwa visa katika jamii vinaweza kuwa viliongezeka kwa hadi asilimia 84, vikichochewa na hatua za kufungwa kwa shughuli, msongo wa mawazo na kutengwa kijamii.
Na hali ya baadaye inaweza kuwa ya kutisha zaidi. Kufikia mwaka wa 2050, idadi ya watu duniani wenye umri wa zaidi ya miaka 60 inatarajiwa kuongezeka maradufu, kutoka milioni 900 mwaka wa 2015 hadi takriban watu bilioni mbili.
Ikiwa viwango vya unyanyasaji vitabaki vilevile, WHO inakadiria kuwa idadi ya waathiriwa inaweza kufikia wazee milioni 320 duniani kote.
WHO inasema unyanyasaji mara nyingi hutokea katika mahusiano yaliyojengwa kwa kuaminiana, jambo linalowafanya waathiriwa washindwe kuripoti kinachoendelea kwa sababu ya hofu ya kumpoteza mtu anayewatunza au hata kutelekezwa.
Kwa nini hali hii hutokea?
Kulingana na ripoti ya WHO, mambo kadhaa huongeza hatari. Wazee wenye ulemavu, tatizo la afya ya akili, afya mbaya ya kimwili, au masikini.
Kwa upande mwingine, wanaohusika kwa unyanyasaji huo wanaweza kuathiriwa na magonjwa ya akili, matumizi mabaya ya dawa za kulevya, utegemezi wa kifedha kwa mzee, au msongo mkubwa wa mawazo ya utunzaji, umri, dhana potofu na ubaguzi dhidi ya wazee, pia huchukua jukumu kubwa, kuruhusu unyanyasaji kubaki siri na kupuuzwa
Athari zake ni zaidi ya makovu.
WHO yaonya unyanyasaji kwa wazee unaweza kusababisha mfadhaiko, wasiwasi, kupungua kwa utambuzi, uharibifu wa kifedha, kupelekwa mapema katika nyumba za wazee na hata vifo vya mapema.
Kwa wazee, kupona mara nyingi huchukua muda, ikimaanisha kuwa makovu ya kimwili na kisaikolojia yanaweza kudumu kwa miaka mingi.
Ili kukabiliana na janga linalokua, WHO na washirika wake wametambua vipaumbele vitano vya kimataifa chini ya Muongozo wa Umoja wa Mataifa wa Uzee Bora.
Hivyo ni pamoja na:
• Kupambana na chuki dhidi ya uzee.
• Kukusanya taarifa bora ili kuelewa tatizo.
• Kupanua programu za kinga zilizothibitishwa.
• Kuwekeza rasilimali zaidi katika kuwalinda wazee.
• Kuongeza ufadhili na uelewa wa kimataifa.
Kama kauli mbiu ya WHO inavyosema:
"Unyanyasaji kwa wazee ni ukiukwaji wa haki za binadamu."
Shirika hilo linasema kuwalinda wazee kunahitaji serikali kuchukua hatua katika mifumo
ya huduma za afya, jamii na familia pia.





















