AFRIKA
2 dk kusoma
Somalia yaimarisha jeshi lake kwa ushirikiano na Rwanda
Mataifa yote mawili yamekubaliana kuhusu usalama katika kanda na fursa za kuimarisha uhusiano wa kijeshi.
Somalia yaimarisha jeshi lake kwa ushirikiano na Rwanda
Ujumbe wa Somalia ulipokelewa katika Makao Makuu ya Jeshi la Rwanda huko Kimihurura. / Wengine
tokea masaa 6

Somalia na Rwanda wamethibitisha dhamira yao ya kuimarisha ushirikiano wa kijeshi kama sehemu ya juhudi za kuhakikisha usalama katika kanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Ujumbe wa jeshi la Somalia ulioongozwa na Mkuu wa Majeshi, Meja Jenerali Odawa Yusuf Rage, ulianza ziara rasmi ya siku sita nchini Rwanda, wakiangazia ushirikiano zaidi kati ya Jeshi la Somalia (SNAF) na Jeshi la Rwanda (RDF).

Meja Jenerali Odawa, ambaye aliteuliwa tena kuwa mkuu wa majeshi ya Somalia Novemba 2024, ameandamana na maafisa waandamizi wa Somalia, ikiwemo Luteni Kanali Iimaan Elman, Mkuu wa ushirikiano kati ya Raia na Jeshi (CIMIC) katika jeshi la Somalia.

Wakati wa ziara hiyo, ujumbe wa Somalia unatarajiwa kutembelea taasisi muhimu za jeshi nchini Rwanda chini ya Wizara ya Ulinzi, pamoja na Makumbusho ya mauaji ya kimbari, ikiwa sehemu ya mafunzo kuhusu taasisi za elimu na uponyaji baada ya vita.

Siku ya Jumanne, ujumbe wa Somalia ulipokelewa katika Makao Makuu ya Jeshi la Rwanda eneo la Kimihurura, ambapo Meja Jenerali Odawa alifanya mazungumzo na Waziri wa Ulinzi wa Rwanda, Juvenal Marizamunda, na Mkuu wa Majeshi, Jenerali M.K. Mubarakh. Mazungumzo yao yaliangazia usalama katika kanda na fursa za kuimarisha uhusiano wa kijeshi.

Ujumbe huo pia ulitembelea makumbusho ya mauaji ya kimbari ya Kigali, ambapo walitoa heshima zao kwa waliouawa katika mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi, wakiweka msisitizo kwa dhamira za mataifa yote mawili kushirikiana katika masuala ya amani na maridhiano.

Ziara ya Mkuu wa Majeshi ya Somalia inakuja wakati nchi hiyo ikiendelea kufanya mabadiliko katika sekta yake ya ulinzi na kuimarisha uhusiano na washirika katika kanda chini ya mpango wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

CHANZO:TRT Afrika Swahili