Ufaransa inajiandaa na maandamano ya siku mbili yatakayofanyika siku ya Alhamisi.
Takriban watu 800,000 wanatarajiwa kushiriki maandamano hayo, ambapo raia wa nchi hiyo, wanalalamikia mwelekeo wa nchi hiyo.
Barabara mbalimbali pamoja na huduma za treni pamoja na shule, zinatarajiwa kufungwa siku ya Alhamisi, kupisha maandamano hayo.
Maandamano hayo yanakuja wiki moja baada ya Rais Emmanuel Macron kumteua mtu wake wa karibu Sebastien Lecornu kama Waziri Mkuu kutatua kasoro za kisiasa nchini humo.
Jumatano iliyopita, waandamanaji wapatao 200,000 walijitokeza mitaani kuonesha kutokufurahishwa kwao na namna Macron anavyoiendesha nchini hiyo.
Maandamano ya Alhamisi yanatajwa kufanana na yale ya mwaka 2023, ambayo yalipinga mageuzi tata kwenye mfumo wa mafao ambapo watu wapatao milioni moja walishiriki.
Waziri wa Mambo ya Ndani anayemaliza muda wake, Bruno Retailleau, aliwaambia walinda usalama juu ya uwezekano wa kutokea kwa vurugu wakati wa maandamano hayo, kutokana na uwepo wa vikundi vidogo vidogo vya wahuni.