Matumizi ya mitandao ya kijamii kwa watoto yanaendelea siku hadi siku duniani.
Mbali na kutumia mitandao katika mawasiliano, kujenga urafiki na kama njia ya kujifunza, mitandao hiyo pia imewaweka kwenye hatari zaidi za manyanyaso ya kijinsia mitandaoni.
Katika baadhi ya nchi za Afrika, kama vile Kenya, tafiti zinaonesha ukubwa wa tatizo.
Kwa mfano, Kituo Maalumu cha Watoto Waliopotea (NCMEC) kilikuwa na taarifa zaidi ya 46,000 za manyanyaso ya kijinsia dhidi ya watoto kwa mwaka 2023.
Kulingana na utafiti uliofanywa na Terre des Hommes Netherlands, asilimia 47.7 ya watoto katika ukanda wa Afrika Mashariki wanakabiliwa na matukio ya unyanyasaji mitandaoni.
Taarifa hizi zinashtua.
Hizi si tafiti tu, bali ni simulizi zenye kuumiza moyo kwa walio wasio na hatia.
Ukatili wa kijinsia mitandaoni umeacha makovu makubwa na athari za kisaikolojia pamoja na kijamii.
Uelewa wa matumizi ya mitandao
Ripoti ya mwaka 2025 ya ukatili wa kijinsia inaonesha kuwa wazazi wengi wamekosa uelewa wa kimsingi wa namna za kuwalinda watoto wao dhidi ya vitisho vya mitandaoni.
Wengi wamekiri kutokuwa na uelewa wa namna mitandao ya jamii inavyofanya kazi, wakati wengine wakisema kuwa ni nadra sana kwao kuzungumzia hatari za mitandaoni na watoto wao.
Hata hivyo, jambo la kutia moyo, ni kuona baadhi ya wazazi wakionesha utayari wa kuongeza uelewa kwenye masuala ya kidijiti na kuzungumza na watoto wao juu ya usalama wao mitandaoni.
Mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia mitandaoni ni jambo la muhimu kwa kila mtu. Kwa upande wao, serikali zinabidi kuonesha mfano, kwa kuzipa nguvu sheria zilizotungwa na kutenga bajeti kwa ajili ya ulinzi wa watoto.
Vile vile, watoa huduma za kimtandao wanapaswa kuwa na nyenzo za kuwalinda watoto dhidi ya ukatili kwenye majukwaa yao, na kuondoa kabisa maudhui yenye kuwaweka watoto kwenye hatari ya kukabiliana na ukatili huo.
Kwa upande wao, ni muhimu kwa watoto kuwa na majukwaa yao maaluu ya kuzungumza.
Toka mwaka 2022, mradi wa SCROL unaotekelezwa na Terre des Hommes Netherlands, umefanya kazi maeneo mbalimbali kama vile Nairobi, Kisumu, na Kisumu, kwa nia ya kufanya mazingira ya kidijiti yawe salama kwa matumizi ya watoto.
Mafanikio
Ndani ya miaka mitatu, Kenya imekuwa na mafanikio makubwa katika kutoa ulinzi wa watoto mitandaoni, kupitia ushirikiano imara baina ya serikali, wasimamizi wa sheria, asasi za kiraia na sekta binafsi.
Mradi huo umejenga uratibu wa kitaifa ambapo kila sekta itakuwa na nafasi yake.
Hadi kufikia leo, wasimamizi wa sheria wanashughulika na matukio ya ukatili mitandaoni kwa tahadhari na weledi mkubwa.
Mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano kati ya Mahakama na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka, huku kasi za uchunguzi wa matukio hayo ikiwa imeongezeka.
Katika ngazi ya jamii, wazazi na walezi wamekuwa na uelewa mkubwa huku watoto wakitumia majukwaa salama kama vile Childline 116.
Licha ya mafanikio haya, bado watoto wanaendelea kukumbwa na manyanyaso mitandaoni.
‘Sikilizeni na mchukue hatua’
Wakati wa mkutano wa watoto wa mwaka 2025 uliofanyika Afrika Kusini, watoto kutoka Kenya, waliungana na wenzao ulimwenguni, wakitaka kutambuliwa kwa usalama wa mitandaoni.
Ujumbe wao mkuu ulikuwa: Mtusikilize na mchukue hatua.
Uelewa pekee hautoshi. Masuluhisho endelevu yanahitajika, yenye kushirikisha serikali na sekta binafsi na kuhakikisha upatikanaji wa misaada ya kisaikolojia kwa waathirika.
Licha ya kuwepo kwa mafanikio, changamoto za Akili Mnemba na udhaifu kwenye ufuatiliaji unachelewesha mwenendo wa kesi mahakamani.
Serikali duniani kote lazima zitenge rasilimali na bajeti zaidi kwa ajili ya ulinzi wa mtoto mtandaoni na kujumuisha OCSE katika mitaala ya elimu kama stadi kuu ya maisha.
Kampuni za teknolojia zinahitaji kwenda zaidi ya sera na kuhakikisha usalama-kwa-usanifu kwa watoto. Wazazi lazima wawe macho na watendaji katika kuhakikisha usalama wa watoto wao katika anga ya kidijitali.
Sekta ya kibinafsi na jumuiya za kiraia lazima zidumishe na kuongeza maendeleo yaliyofanywa chini ya miradi kama ule wa SCROL kwa kuwekeza katika mifumo imara, sera na ushirikiano unaomlinda kila mtoto mtandaoni.
Hakuna mtoto anayepaswa kudhulumiwa, mtandaoni au nje ya mtandao. Ni lazima tuwalinde Watoto Wote dhidi ya Unyanyasaji wa Ngono kwa Watoto Mtandaoni.
Mwandishi wa maoni haya, Magdalene Wanza, ni Mkurugenzi Mkazi wa taasisi ya Terre des Hommes Netherlands.
















