Watu wapatao 123 wamepoteza maisha na wengine 130 hawajulikani walipo nchini Sri Lanka kufuatia kimbunga kilichoikumba nchi hiyo.
Katika wilaya ya Kandy, viliripotiwa vifo 51 huku wengine 67 wakiwa hawajulikani walipo.
Wakati huo huo, katika eneo la Badulla, watu 35 waliripotiwa kufa, kulingana na chombo cha habari cha eneo hilo.
Inaripotiwa kuwa, kimbunga hicho kilichotokea Novemba 26, kiliathiri jumla watu 373,428 kutoka kaya 102,877, huku wengine 43, 925 wakipatiwa maeneo maalumu ya hifadhi.
Hali mbaya ya hewa, ikiwemo mvua kubwa na maporomoko ya ardhi, imeendelea kuikumba kisiwa hicho toka Novemba 17, mwaka huu.
Tayari, mamlaka za nchi hiyo zimetoa tahadhari za uwezekano wa kutokea kwa mafuriko makubwa, wakiwataka watu waishio maeneo ya mabondeni kukimbilia kwenye maeneo ya usalama.
Rais wa Sri Lanka Anura Kumara Dissanayake ameagiza vikosi vya wanajeshi 20,000 kuanza shughuli za uokozi katika maeneo yaliyoathirika zaidi.

















