AFRIKA
2 dk kusoma
DRC yawaachia huru zaidi ya raia 50 wa Somalia baada ya juhudi za kidiplomasia
Kuachiwa kwao kulitokea siku tatu baada ya Balozi Hassan kukutana na viongozi wa DRC na kuwasilisha ombi rasmi kwa niaba ya serikali ya Somalia.
DRC yawaachia huru zaidi ya raia 50 wa Somalia baada ya juhudi za kidiplomasia
Rais wa DRC, Felix Tshisekedi./Picha:Reuters
30 Septemba 2025

Mamlaka nchini DRC imewaachia huru zaidi ya raia 50 wa Somalia waliokuwa wamekamatwa katika jiji la Lubumbashi kufuatia msako wa kiusalama wa raia wa kigeni uliofanyika hivi karibuni.

Watu hao walikamatwa mapema mwezi Septemba, wakati wa operesheni ya kiusalama inayohusiana na uhamiaji katika jiji la Lubumbashi, jiji la pili kwa ukubwa na kitovu muhimu cha kiuchumi nchini DRC.

Kuachiliwa kwao kulifanikishwa baada ya hatua za haraka za kidiplomasia zilizochukuliwa na serikali ya Somalia.

Akithibitisha habari hizo, Balozi wa Somalia nchini Tanzania ambaye pia analiwakilisha taifa hilo nchini DRC, Ilyas Ali Hassan, alisema kuwa watu hao walikamatwa kimakosa.

Kuachiwa kwao kulifanyika siku tatu baada ya Balozi Hassan kukutana na viongozi wa DRC na kuwasilisha ombi rasmi kwa niaba ya serikali ya Somalia.

“Tunaushukuru uongozi wa serikali rafiki ya Congo, pamoja na jamii ya Wasomali nchini Congo,” alisema Balozi Hassan katika mahojiano yake na TRT Afrika.

Balozi huyo pia aliipongeza jamii ya Wasomali iishiyo nchini DRC kwa kudumisha sifa njema kwa kutii sheria za nchi mwenyeji na aliwahimiza kuendelea kufuata kanuni za nchini humo huku wakiheshimu mamlaka ya DRC.

Tukio hilo linatokea wakati uhusiano kati ya nchi hizo mbili ukizidi kuimarika, hasa baada ya Somalia kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Somalia ilikubaliwa rasmi kuwa nchi mwanachama wa 8 wa jumuiya hiyo mwezi Machi 2024, ikijiunga na Burundi, DRC, Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Uganda, na Tanzania.

Licha ya uanachama wake wa EAC, raia wa Somalia wanakabiliwa na vikwazo vya viza na uhuru wa kutembea ndani ya jumuiya hiyo.

CHANZO:TRT Afrika Swahili