Mashambulizi ya wapiganaji wa RSF nchini Sudan katika hospitali moja kwenye mji wa Al-Fasher yamewaua watu 20 ndani ya saa 24, vyanzo vya maafisa wa afya vimesema siku ya Jumatano.
Wale waliouawa ni pamoja na maafisa wawili wa afya, wenzao wa Hospitali ya Al-Fasher wameiambia AFP kwa masharti ya kutotambuliwa.
Mashambulizi ya Jumanne na Jumatano yamesababisha "uharibifu mkubwa kwa majengo ya hospitali" na kuwajeruhi watu 24.
Siku ya Jumanne, mashambulizi ya ndege zisizokuwa na rubani katika wadi ya wajawazito,yaliwaua watu wanane.
Hospitali zinashambuliwa kila mara
Mashambulizi ya makombora siku ya Jumatano yaliwaua watu 12 zaidi.
Hospitali nyingi mjini Al-Fasher zimeshambuliwa kwa mabomu kila mara na kulazimika kufungwa, kuacha karibu asilimia 80 ya watu wa mji huo wakihitaji huduma ya afya lakini hawana njia ya kufikia huduma hiyo, kulingana na Umoja wa Mataifa.
Kote nchini, hospitali zimekuwa zikishambuliwa mara kwa mara, kuvamiwa na wapiganaji na kuporwa, huku chama cha madaktari kikisema kuwa asilimia 90 ya hospitali kwa wakati fulani zimelazimika kufungwa.
Wahudumu kadhaa wa afya wameripotiwa kuuawa, ikiwemo kile ambacho Umoja wa Mataifa kinasema mashambulizi yaliyowalenga kwa makusudi.