Ethiopia yapanga kuvunja rekodi ya miti mingi iliyopandwa ndani ya siku moja

Ethiopia yapanga kuvunja rekodi ya miti mingi iliyopandwa ndani ya siku moja

Kampeni ya upandaji miti inalenga kurejesha misitu nchini ambayo imepungua kwa kiasi kikubwa katika miaka mingi
Ethiopia ilizindua mradi wa upandaji miti ili kukabiliana na ukataji miti. / Picha: AA

Ethiopia inalenga kuvunja rekodi yake ya kupanda idadi kubwa zaidi ya miti katika siku moja kama sehemu ya kampeni yake ya kukabiliana na athari za ukataji miti na mabadiliko ya hali ya hewa

Walivunja rekodi hiyo mwezi Julai 2019 kwa kupanda miti milioni 353 katika kipindi cha saa 12 tu, kulingana na maafisa, na wanatumai kuzidi kiwango hicho siku ya Jumatatu.

"Lengo letu ni kuvunja rekodi yetu!" Waziri Mkuu Abiy Ahmed alitweet.

"Ushindani wetu ni ya sisi wenyewe. Tunafikiri mikoa, maeneo, wilaya, na vijiji itavunja rekodi zao kwa kupanda zaidi ya mwaka jana. Kila mmoja wetu lazima avunje rekodi zetu wenyewe," aliongeza.

Guinness World Records bado haijathibitisha rekodi ya Ethiopia.

Rekodi ya sasa ya ulimwengu ya miti iliyopandwa katika siku moja inashikiliwa na India baada ya watu zaidi ya 800,000 kupanda miti milioni 50 mwaka 2016 katika jimbo la Uttar Pradesh kaskazini mwa nchi.

Kampeni ya Ethiopia inalenga kurejesha ardhi ya misitu ya nchi ambayo imepungua kutoka asilimia 35 ya eneo lote mwishoni mwa karne ya 19 hadi karibu asilimia 4 katika miaka ya 2000, kulingana na Umoja wa Mataifa.

TRT Afrika