Nchi za kijeshi zilizoshirikiana za Sahel zilikosoa kutua ya dharura kwa ndege ya kijeshi ya Nigeria kutua huko Burkina Faso Jumatatu, huku zikitishia kuchukua hatua ya pamoja dhidi ya ukiukaji wa sheria za anga yao.
Muungano wa Nchi za Sahel — unaojumuisha Mali, Niger na Burkina Faso — ulisema katika taarifa ya pamoja kwamba ndege hiyo ilikuwa na askari wa kijeshi 11 na haikuwa na idhini ya kuruka juu ya anga ya Burkina Faso.
“Ndege inayomilikiwa na Jeshi la Anga la Jamhuri ya Muungano ya Nigeria, aina C-130, ililazimishwa kutua leo Bobo Dioulasso, Burkina Faso, baada ya tukio la dharura lililotokea wakati ikifanya operesheni katika anga ya Burkinabe,” ilisema taarifa ya muungano iliyosomwa katika vyombo vya habari vya serikali katika nchi tatu za Afrika Magharibi.
Taarifa ilikitaja kitendo hicho kuwa “sio cha kirafiki” na kusema majeshi ya anga ya nchi hizo yameruhusiwa kukabiliana na uvunjifu wowote wa sheria za anga katika eneo hilo.
Taarifa ya pamoja haikueleza kilichotokea kwa askari hao 11 waliokuwa ndani ya ndege ya Nigeria.
Nchi tatu za Sahel, zinazopambana na makundi ya kigaidi katika eneo la Sahel, zinahifadhi uhusiano wa mvutano na majirani zao wa Afrika Magharibi. Mnamo Januari, walijitoa katika umoja wa ECOWAS baada ya kuunda muungano wao wenyewe.
Nchi hizo pia zimejitenga na baadhi ya nchi za Magharibi, hasa mkoloni wa zamani Ufaransa, huku zikijaribu kuimarisha uhusiano na Urusi.















