Marekani na madola ya Ulaya yametoa wito kwa wanajeshi wa Rwanda na wapiganaji wa M23 kusitisha mara moja mashambulizi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, siku chache baada ya marais wa nchi hizo kutia saini makubaliano mjini Washington.
Kundi hilo linaloongozwa na Marekani lilionyesha "wasiwasi mkubwa" kuhusu mapigano karibu na Burundi na kusema kuwa yana "uwezo wa kuvuruga utulivu kwa eneo zima."
Taarifa ya pamoja ilisema muungano huo "unawataka M23 na Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) kusitisha mara moja operesheni zao za mashambulizi mashariki mwa DRC, hasa Kivu Kusini, na kutoa wito kwa RDF kujiondoa mashariki mwa DRC." Rwanda imekanusha mara kwa mara ripoti za kufanya kazi pamoja na M23 ili kuchochea ukosefu wa utulivu mashariki mwa DRC.
Taarifa ya pamoja iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani pia inatoa wito kwa M23 "kurejea kwenye nyadhifa zake na kutekeleza... ahadi za Azimio la Kanuni" zilizofikiwa katika mazungumzo na serikali ya Kinshasa yaliyofanyika Qatar mwezi Julai.
Tishio la mzozo
Umoja wa Ulaya pia ulitia saini taarifa hiyo.
Marais hao wa Rwanda na DRC walikuwa wametia saini makubaliano siku ya Alhamisi mjini Washington mbele ya Rais wa Marekani Donald Trump.
Hata hivyo, DRC na nchi jirani ya Burundi wamepaza sauti zao katika siku chache tangu wakati huo kwani waasi wa M23 wameshambulia maeneo ya mpakani.
Taarifa ya pamoja ya Marekani na EU pia ilionyesha "wasiwasi hasa wa kuongezeka kwa matumizi ya ndege zisizo na rubani katika mzozo."
"Hii inawakilisha ongezeko kubwa la mapigano na inaleta hatari kubwa kwa raia," ilisema.









