Miche Minnies and Ronaldinho

Miche Desiree Minnies wa Afrika Kusini ambaye sura yake imefanana na mchezaji wa mpira nguli wa soka wa Brazil Ronaldinho Gaucho, na ulimwengu umelichukua jambo hilo kwa uzito mkubwa na kuteka hisia za watu wengi.

Ulinganisho wa mwonekano huo ulianza wakati jukwaa la mpira wa miguu, 433, lilipoandika kwenye Instagram kwamba Minnies, 21, ameleta kumbukumbu za kupendeza za "mtu fulani."

Zaidi ya watumiaji 7,000 wa Instagram walisema kwa kukubaliana kwamba Minnies anafanana sana na Ronaldinho, ambaye alishinda Kombe la Dunia, Ballon d'Or, Tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia wa FIFA na Ligi ya Mabingwa ya UEFA katika maisha yake ya soka ambayo yamesalia kuwa mashuhuri kwa miaka 20.

Minnies anacheza kama mshambuliaji wa klabu ya soka ya Mamelodi Sundowns Ladies yenye makao yake mjini Pretoria, timu ya daraja la juu katika ligi ya wanawake nchini Afrika Kusini.

Mnamo mwaka wa 2018, aliwakilisha Afrika Kusini katika Kombe la Dunia la FIFA la Wanawake chini ya 17 nchini Uruguay.

Katika msimu wa 2021/22, Minnies aliifungia Sundowns mabao 22 ya ligi na kuisaidia klabu hiyo kushinda taji lake la tano la ligi.

Alishika nafasi ya pili katika orodha ya wafungaji bora, nyuma ya mchezaji mwenzake Boitumelo Rabale ambaye alikuwa na mabao 24.

Baadhi ya mashabiki wa soka wametania kwamba Ronaldinho, ambaye ana umri wa miaka 43, anapaswa kuomba uchunguzi wa DNA ili kubaini kama ana uhusiano na Minnies.

Rekodi rasmi za kuzaliwa, hata hivyo, zinaonyesha kuwa Minnies, ambaye alizaliwa Novemba 14, 2001 huko Cape Town, Afrika Kusini, hana ukoo wowote na mchezaji wa zamani wa Barcelona, ​​AC Milan na PSG.

Kabla ya kujiunga na Sundowns mnamo Machi 2022 kwa kandarasi ya miaka minne, Minnies alichezea RSA Vasco Da Gama, klabu inayocheza katika ligi ya wanawake ya mkoa wa nusu-professional.

Katika msimu wa 2020/21, uwezo wake wa kupachika mabao uliifanya klabu ya Vasco Da Gama kushinda ligi ya mkoa wa wanawake na kufuzu hadi daraja la juu.

Mfungaji Bora

Wakati akiondoka Vasco Da Gama kwenda Sundowns, aliyekuwa kocha wa Minnies Ashraf Calvert alisema alijisikia "kufanikiwa" kwa kumsaidia mshambuliaji huyo "kubadilisha maisha yake kuwa bora."

Sundowns, chini ya uongozi wa kocha mkuu Jerry Tshabalala, inafurahia mafanikio nje ya Afrika Kusini pia.

Klabu hiyo ilitawazwa washindi wa Ligi ya Mabingwa ya Wanawake ya Baraza la Vyama vya Soka Kusini mwa Afrika (COSAFA) mnamo 2021 na washindi wa Ligi ya Mabingwa ya Wanawake ya CAF mwaka huo huo.

Mnamo 2022, klabu ilifika fainali ya mashindano yote mawili na kuibuka washindi wa pili.

TRT Afrika