Baraza la Amani na Usalama la Afrika ni chombo kikuu katika Umoja wa Afrika chenye jukumu la kuzuia na kusuluhisha migogoro./Picha: Getty      

Na Edward Qorro

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Likiwa limeanzishwa mwaka 2004, Baraza la Amani na Usalama la Umoja Afrika (AUPSC) linatimiza miaka 20 Mei 25, 2024.

Sherehe hizo zinapangwa kufanyika jijini Dar es Salaam Mei 25, tukio ambalo litatawaliwa na mihadhara, mazungumzo na majadiliano yatakayoendeshwa na jopo la viongozi wastaafu kutoka bara la Afrika, huku dhima kuu ikiwa ni 'Chombo cha Uamuzi, miongo miwili ya Afrika, usalama tunaoutaka'.

“Kutakuwa na majopo mawili yatakayojadili hali ya ulinzi na usalama Afrika kwa miaka 20 iliyopita na mwelekeo kwa miaka ijayo,” amesema January Makamba, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kutoka Tanzania.

Mnamo mwezi machi 2022, Tanzania ilichaguliwa kuhudumu kwenye nafasi ya Mjumbe wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika kwa miaka miwili hadi mwezi Machi 2024 ambapo muda wa kuhudumu ulifikia kikomo.

Miongoni mwa washiriki wa maadhimisho hayo ni Moussa Faki Mahamat ambaye ni mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Makamu wa Rais wa Uganda, Jesca Alupo na rais mstaafu wa Nigeria Olusegun Obasanjo.

Kulingana na Makamba, wengine ni Rais mstaafu wa Tanzania Jakaya Kikwete, Domitien Ndayizeye wa Burundi na Joaquim Chissano wa Msumbiji.

Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat ni mmoja wa wanadiplomasia watakaohudhuria maadhimisho hayo./Picha: TRT Afrika

Kuanzishwa kwa Baraza hilo

Barala la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika lenye wanachama 15 wa kuteuliwa, lina jukumu la kuzuia kutokea kwa migogoro, kusuluhisha au kukabiliana nayo pale inapojitokeza.

Hadi sasa, baraza hilo linasimamia shughuli 10 za kulinda amani katika nchi 17 barani Afrika, likijumuisha walinda amani zaidi ya 70,000.

"Operesheni hizi ni nyenzo muhimu katika zana muhimu za kudhibiti migogoro. Katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, operesheni za amani zinazoongozwa na Waafrika zimefanya jitihada za kushugulikia vitisho vya machafuko barani Afrika," imesomeka sehemu ya chapisho katika tovuti ya African Center for Strategic Studies.

Hadi sasa, baraza hilo linasimamia shughuli 10 za kulinda amani katika nchi 17 barani Afrika, likijumuisha walinda amani zaidi ya 70,000./Picha: AFP

Kwa upande wake, mhadhiri mwandamizi kutoka Chuo cha Diplomasia nchini Tanzania (CFR), Dkt Jason Nkyabonaki anaiambia TRT Afrika kuwa uwepo wa tume hiyo kwa miaka 20 ni ushahidi tosha wa mafanikio yake.

Kulingana na mtaalamu huyo wa diplomasia, mapinduzi ya kawaida yaliyotawala bara la Afrika katika miaka ya 70 na 80, kwa sasa yameanza kupungua kutokana na uwepo wa baraza hilo la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika.

"Baraza hili limejitahidi sana kukomesha matukio ya mapinduzi ya kisiasa barani Afrika, na ndio maana Afrika imekataa kumpongeza Rais wa Chad Mahamat Déby hivi karibuni," ameeleza.

Hata hivyo, Dkt Nkyabonaki anasisitiza uhuru wa kiuchumi ili Afrika iweze kupunguza idadi ya migogoro yake.

"Suala hili halina mjadala kwa sasa, kwa sababu migogoro mingi hutokana na makundi kugombea mgawanyo wa rasilimali."

Hata hivyo, mwanadiplomasia huyo anaona fahari kuona Afrika ikimiliki baraza hilo, likitambua umuhimu wake kwa mustakabali wa bara zima.

TRT Afrika