Muziki wa Amapiano umepata umaarufu miongoni mwa vijana/ Picha: AFP 

Pengine mwimbaji wa Marekani Swae Lee hakujua utata mkubwa aliokuwa akijiingiza ndani alipochapisha habari kwenye mtandao wa twitter akitangaza nyenzo zake mpya za Amapiano Jumanne jioni.

‘’Subiri hadi utamsikia Swae Lee kwenye Amapiano,’’ aliandika kwenye Twitter, na kufuatiwa na ishara ya bendera ya Nigeria.

Amapiano ni tanzu ya muziki iliyochipuka Afrika Kusini katikati ya miaka ya 2010.

Ni mseto wa muziki wa deep house, jazz, na sauti zilizotulia wa mapumziko.

Kitu ambacho Swae Lee hakutarajia ni majibu makali na ya haraka yaliyofuata.

Swae Lee alianzisha mjadala mtandaoni kuhusu asili ya muziki wa Amapiano. Picha: Reuters

Maoni chini ya chapisho lake yalifurika zaidi na Waafrika Kusini ambao walikasirishwa kwamba alithubutu kuashiria kuwa Amapiano ni aina ya muziki sawa na Nigeria.

Katika muda wa chini ya saa moja, zaidi ya maoni 3,900 yalimimimika katika mtandao wake, na kuingia katika mada iliyojadiliwa vikali.

‘’ Amapiano ni ya Afrika Kusini; fanya utafiti wako,'' alitweet mtu mmoja wa anwani ya @SA Hip Hop 247. ‘’Huyu ni msanii wa pili wa kimataifa kufanya kosa hili,’’ aliandika @iamdavejr aliyekasirishwa.

‘’Wapendwa Waafrika Kusini, haijalishi unafanya nini au useme nini, haitabadilisha ukweli kwamba Nigeria ilishawishi Amapiano kuwa jinsi ilivyo sasa. Hakuna aliyejua ni nini hadi Wizkid na Davido walipourukia ,’’ aliandika Oghenerie pia kwaTwitter.

Huku malumbano hayo yakivuma na kuwa mada motomoto na maarufu, Swae Lee alirejea kwenye mitandao ya kijamii ili kuondoa hali hiyo.

‘’Sijawahi kumdharau mtu yeyote. Samahani nyote ambao mmeiona hivyo. Sikuwahi kusema chochote kuhusu asili yake katika ujumbe wangu kwa tweeter na siondoi Amapiano kutoka kwa mtu yeyote," aliandika.

Swae Lee alizidi kusema kuwa kwa kiasi fulani yeye ni Mnigeria, na ndiyo sababu alikuwa ametumia bendera.

Lakini wasiwasi wake mkubwa ni mgawanyiko unaoonekana kati ya Waafrika, ambao anasema muziki bado haujaponya.

‘’Nadhani hili limenifungua macho tu kuona matatizo mengi tuliyo nayo, unajua, mgawanyiko huu... Kuna nini kuhusu mgawanyiko huu? Tunahitaji kujumuika na kupeana nguvu,’’ aliomba katika video iliyofuata iliyochapishwa kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Mijadala ya siku za nyuma ilikuwa mikali kwa sababu watu mashuhuri walijumuika na kuchukua pande tofauti za mabishano.

Muziki wa Amapiano una sifa ya midundo na densi kwa nguvu Picha: AFP

Mwaka jana, Davido alipinga maoni yaliyotolewa na DJ Maphorisa baada ya kumshutumu shabiki huyo, na hivyo kuwasha moto na kuzua mjadala mkali uliodumu kwa siku kadhaa.

Huenda DJ Maphorisa alipata funzo baada ya hapo na sasa ametuma ujumbe mzito kwa mashabiki wote wa Amapiano duniani kote:

‘’Amapiano ni yetu sote,’’ aliandika ujumbe kwa twitter, Jumatano huku majibizano yakiendelea kwenye mitandao ya kijamii.

Amapiano bado ni aina kubwa ya mauzo ya nje inayotoka Afrika, ikiwa na karibu mitiririko bilioni mbili kwenye Spotify.

TRT Afrika