Na Charles Mgbolu
Watumbuizaji wa Kiafrika wanatarajiwa kuubeba mwenge wa bara hili kwa fahari katika tuzo za mwaka huu za Black Entertainment Television (BET).
Tukio la mwaka huu limepangwa kufanyika katika ukumbi wa Microsoft Theatre katika jiji la Los Angeles nchini Marekani 24 Juni huku wasanii tisa wa Kiafrika wakiwania tuzo katika vipengele sita vya muziki.
Ni dhifa ya kila mwaka ya Marekani iliyoanzishwa na mtandao wa Black Entertainment Television mwaka wa 2001 ili kusherehekea watumbuizaji weusi na watu wanaobaguliwa katika muziki, filamu, michezo, na uhisani.
Burna Boy, Wizkid, Tems, Ayra Starr, na Asake, wote kutoka Nigeria, pamoja na Ntokozo Mdluli K.O. na Pabi Cooper kutoka Afrika Kusini, Camidoh kutoka Ghana, Libianca kutoka Cameroon, na Uncle Waffles kutoka Etswatini wameteuliwa katika vipengele tofauti.
Damini Ebunoluwa Ogulu, anayejulikana pia kama Burna Boy, hata hivyo, anaongoza kundi hilo kwa kuteuliwa katika vipengele vinne: Msanii Bora wa Kiume wa R&B/Pop, Muigizaji Bora wa Kimataifa, Chaguo la Watazamaji, na mzalishaji bora wa Video wa Mwaka.
" Inapendeza kuona Waafrika wakipiga hatua kuu katika tuzo za kimataifa za burudani za aina hii. Wasanii hawa wanastahili kwa sababu wamejitahidi sana kufika hapa,’’ Chuks Nwanne, mhariri wa gazeti la The Guardian la Nigeria, aliiambia TRT Afrika.
Wasanii wa Kiafrika wamekuwa wakitajwa mara kwa mara kuwania tuzo za kimataifa za burudani na mara nyingi walitwaa tuzo hizo.
Mbio Kali
Katika kipengele cha Msanii Bora wa Kiume wa R&B/Pop, Burna Boy, 31, atachuana na watumbuizaji wa uzito wa juu kama vile Chris Brown, Drake, The Weeknd, Usher, Blxstm, na Brent Faiyaz.
Burna ameshinda Tuzo za BET za msanii bora wa Kimataifa kwa miaka mitatu mtawalia (2019, 2020, na 2021).
Lakini mwaka huu unaweza kuwa na changamoto zaidi kwake kwani amepanda hadi kwenye kipengele cha Msanii Bora wa Kiume chenye ushindani zaidi ambacho msanii wa Afrika hajawahi kushinda.
Nyota Kubwa
Mwimbaji na mtunzi wa nyimbo wa Nigeria Temilade Openiyi (Tems), 28, pia yuko katika kitengo cha tuzo za kifahari - Msanii Bora wa Kike wa R&B/Pop.
Hata hivyo, lazima pia ashindane na watumbuizaji wakubwa kama Beyoncé, ambaye wengi wanamwona kama nyota wa kike wa muziki.
Beyoncé amekuwa na mwaka mzuri wa muziki baada ya kuanza kufanya ziara ya kimataifa inayoendelea, ambayo imekuwa ikikosolewa na mashabiki wengi barani Afrika kwa sababu alilipuuza bara katika ratiba yake.
Msanii wa muziki wa kufoka wa Afrika Kusini Ntokozo Mdluli, anayejulikana kitaalamu kama K.O. ameteuliwa katika kipengele cha mwanamuziki bora kimataifa mwaka huu pamoja na Lungelihle Zwane (Uncle Waffles) kutoka Eswatini.
Lakini Tems wa Nigeria hakuteuliwa mwaka huu katika kitengo hiki kilichojumuisha pia Ayra Starr, Burna Boy, wasanii wa Uingereza Stormzy, Ella Mai, Central Cee, na L7nnon kutoka Brazili, na Tiakola kutoka Ufaransa.
Wengine ni mwimbaji wa Afrobeats Libianca kutoka Cameroon, anayejulikana kwa wimbo wake wa kuchupika "People," na mwanadensi na mtayarishaji Pabi Cooper kutoka Afrika Kusini.