Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, siku ya Jumatatu alikataa pendekezo la Rais wa Marekani Donald Trump la kurejea kwenye mazungumzo, na pia alikanusha madai ya Trump kwamba Marekani imeharibu uwezo wa nyuklia wa Iran.
"Trump anasema yeye ni mtaalamu wa kufanikisha makubaliano, lakini kama makubaliano hayo yanaambatana na shinikizo na matokeo yake tayari yameamuliwa, basi hiyo siyo makubaliano bali ni kulazimisha na vitisho," alisema Khamenei kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali.
Wiki iliyopita, Trump aliambia bunge la Israel kuwa ingekuwa vyema iwapo Washington ingeweza kufanikisha "makubaliano ya amani" na Tehran, kufuatia kuanza kwa usitishaji mapigano Gaza kati ya Israel na kundi la wanamgambo wa Kipalestina, Hamas.
Trump pia alisisitiza kuwa Marekani "imeharibu kabisa" maeneo ya nyuklia ya Iran wakati wa mashambulizi hayo.
"Rais wa Marekani anajivunia kusema kuwa wamebomoa na kuharibu sekta ya nyuklia ya Iran. Vizuri, endeleeni kuota!" Khamenei aliongeza.
"Aidha, Marekani inahusikaje kama Iran ina vituo vya nyuklia au la? Mambo haya ni ya kuingilia, ni makosa na ni ya kulazimisha kwa nguvu."
Mataifa ya Magharibi yanaituhumu Iran kujaribu kutengeneza bomu la nyuklia kisiri kupitia mpango wa uzalishaji wa uranium, na yanataka Iran kusitisha shughuli hizo.
Hata hivyo, Tehran inakana kuwa na nia ya kijeshi, ikisisitiza kuwa mpango wake wa nyuklia ni kwa ajili ya matumizi ya nishati ya kiraia pekee.