Saudi Arabia ilisema takriban mahujaji wa Kiislamu milioni 1.2 wamewasili katika ufalme huo kwa ajili ya hija ya kila mwaka .
"Takriban waumini milioni 1.2 walipokelewa katika misikiti miwili mitakatifu," Sheikh Abdulrahman al-Sudais, Imam mkuu wa msikiti wa Makka, alisema katika taarifa zilizotajwa na shirika la habari la serikali SPA.
"Hii ndiyo idadi kubwa zaidi ya waumini nchini Saudi Arabia tangu janga la Uviko-19 ," aliongeza.
Saudi Arabia inatarajia kupokea zaidi ya mahujaji wa Kiislamu milioni mbili kwa ajili ya hija mwaka huu.
Ufalme huo wenye utajiri wa mafuta ulipunguza idadi ya mahujaji katika miaka mitatu iliyopita kutokana na vikwazo vilivyowekwa ili kudhibiti mlipuko wa Uviko-19.
Mnamo 2022, zaidi ya mahujaji waislamu 899,999 walitembelea Saudi Arabia kutekeleza ibada hiyo, kulingana na takwimu rasmi.
Mnamo 2021, ufalme huo ulikaribisha hadi mahujaji 60,000 kutoka ndani ya Saudi Arabia huku kukiwa na vizuizi vya Uviko-19, wakati ni 10,000 pekee waliofanya ibada hiyo mnamo 2020.
Hija katika eneo takatifu la Uislamu la Kaaba huko Makka, ni moja ya nguzo tano za Uislamu.
Waislamu wanatakiwa kufanya hivyo angalau mara moja katika maisha yao kwa mwenye uwezo.




















