Kenya imetangaza msamaha wa deni la kodi kwa maelfu ya raia watakajaza fomu zao za kodi ndani ya muda uliotolewa wa Juni 30.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya ukusanyaji kodi nchini Kenya KRA, msamaha huu unatolewa kwa masharti.
"Msamaha wa ushuru unatumika kwa muda wa hadi Desemba 31 2022, kwa masharti kwamba ushuru wote asili ulipwe na marejesho yote yanayosubiri au ambayo hayajawasilishwa yawasilishwe," ilisema KRA.
Mamlaka ilibainisha kuwa msamaha huo unatumika tu kwa walipa kodi waliotozwa faini au kwa malimbikizi ya riba almuradi wawe wamelipa kodi asili inayodaiwa na wale walio na mrejesho wa kodi ambao hawajawasilisha na wale walio na ushuru asili ambao haujalipwa hadi kufikia 31 Disemba 2022.
KRA ilianzisha mpango huo wa msamaha mwaka jana kufuatia kupitishwa kwa Sheria ya Fedha, 2023, ikilenga kupunguza malipo ya jumla ya madeni kupitia ukusanyaji wa madeni na kuongeza mapato yanayokusanywa kutokana na msamaha.
Pia inalenga kuonesha nia safi kwa upande wa serikali ili kuwahimiza Wakenya zaidi kufanya mrejesho wa ulipaji kodi katika muda muafaka.
Hata hivyo KRA, ilionya kuwa baada ya Juni 30, 2024, adhabu, faini na riba zozote zinazohusiana na ushuru asili ambao haujalipwa au marejesho ambayo hayajajazwa hazitaondolewa.



















