| Swahili
AFRIKA
3 DK KUSOMA
Rais Ramaphosa amkaimisha madaraka Waziri wa Ulinzi
Uamuzi huo unakuja wakati Rais Cyril Ramaphosa akihudhuria mkutano wa SADC huko Zimbabwe.
Rais Ramaphosa amkaimisha madaraka Waziri wa Ulinzi
Rais Ramaphosa yuko nchini Zimbabwe kwa mkutano wa kikanda wa SADC./Picha:Reuters / Reuters
17 Agosti 2024

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amemkaimisha madaraka Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo Angie Motshekga, baada ya kiongozi huyo kuwa anahudhuria mkutano wa kanda ya SADC unaofanyika nchini Zimbabwe, ofisi ya Rais ya nchi hiyo imesema katika mtandao wake, siku ya Jumamosi.

Ramaphosa tuko jijini Harare, akihudhuria Mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Kulingana na katiba ya Afrika Kusini, kiongozi mwandamizi katika serikali atakaimishwa madaraka ya urais wakati Rais yuko nje ya nchi.

Ofisi ya Rais wa Afrika Kusini imesema kuwa Angie Motshekga ataiongoza nchi hiyo kipindi chote Ramaphosa akihudhuria mkutano huo nchini Zimbabwe.

Hii ni mara ya pili kwa Motshekga kukaimu nafasi hiyo ya juu nchini humo, mara ya kwanza ikiwa ni mwaka 2021 wakati Rais Ramaphosa alipohudhuria mazishi ya Rais wa zamani wa Zambia, Kenneth Kaunda.

Hatua ya Rais Ramaphosa inakuja baada ya kuchaguliwa kwa serikali ya kwanza ya mseto nchini humo tangu kumalizika kwa utawala wa kibaguzi mwaka 1994.

Serikali ya Mseto

Chama cha ANC, ambacho kimekuwa kikiongoza Afrika Kusini tangu kuangushwa kwa utawala wa kibaguzi, kilipoteza wingi wake wa wabunge kwa mara ya kwanza katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Mei, na kukilazimisha kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa na vyama vingine vya siasa.

Hali ya kisiasa katika moja ya mataifa yenye uchumi mkubwa zaidi barani Afrika imesalia kuwa ya wasiwasi tangu uchaguzi, huku ushindani kati ya Rais wa zamani Jacob Zuma na Ramaphosa ukiendelea.

Ajenda za mkutano

Wakuu wa nchi za SADC wanakutana jijini Harare kwa mkutano wa 44 wa kanda hiyo.

Mkutano huo unafanyika chini ya kaulimbiu "Kukuza ubunifu ili kufungua fursa za ukuaji endelevu wa uchumi na maendeleo kuelekea SADC ya viwanda."

Mkutano huo utashuhudia Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe akichukua nafasi ya mwenyekiti wa jumuiya hiyo yenye wanachama 16, akichukua nafasi ya Rais wa Angola Joao Lourenco.

Mkutano huo pia unatarajiwa kujadili suala linaloongezeka la milipuko wa ugonjwa wa mpox katika mataifa kadhaa barani Afrika pamoja na amani na usalama wa kikanda.

Pata habari zaidi kupitia Whatsapp channels

CHANZO:TRT Afrika