Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan amesema kuwa Uturuki inatarajia kundi la kigaidi la YPG litaheshimu makubaliano ya Machi 10 nchini Syria na kutimiza wajibu wake haraka iwezekanavyo.
“Vita dhidi ya ugaidi lazima viendelee kwa njia thabiti zaidi. Tunatarajia YPG itaheshimu makubaliano ya Machi 10 na kutimiza wajibu wake haraka iwezekanavyo,” Fidan alisema siku ya Ijumaa.
Fidan pia alisisitiza kuhusu umuhimu wa kuhakikisha utulivu nchini Syria kwa ajili ya amani na maslahi ya watu.
“Leo, tumejadiliana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria, Asaad al Shaibani. Tunafuatilia kwa karibu na hatua zilizopigwa hivi karibuni,” aliongeza.
Uhasama kuzidi Aleppo
Kulingana na takwimu za nchini Syria, raia zaidi ya 3,000 wameondoka katika maeneo yao kutokana na mashambulizi ya magaidi wa YPG.
Vurugu hizi zimelazimisha uongozi wa mkoa huko Aleppo kutangaza kuendelea kufungwa kwa shule za umma na binafsi pamoja na vyuo vikuu kwenye mji huo siku ya Alhamisi.
Machi 10, ofisi ya rais wa Syria ilitangaza kutiwa saini kwa makubaliano ya kujumuisha YPG katika taasisi za serikali, kusisitiza kuhusu umoja wa nchi hiyo na kukataa majaribio yoyote ya kuleta mgawanyiko.
Mamlaka nchini Syria zinasema kuwa miezi kadhaa tangu wakati huo, YPG haijaonesha juhudi za kutekeleza yaliyokuwemo kwenye makubaliano hayo.
Serikali ya Syria imezidisha juhudi za kuhakikisha usalama kote nchini tangu kuondolewa madarakani kwa utawala wa Bashar al Assad Disemba 8 2024, baada ya kuwepo uongozini mwa miaka 24.




















