Mgogoro wa Israel na Iran umezua tishio la Iran kufunga mlango wa bahari wa Hormuz unaotumika kupitisha takriban mapipa milioni 20 ya mafuta kwa siku.
Hili limezua mjadala kuhusu uwezo wa Afrika wa kujitosheleza kwa uzalishaji wake.
Kulingana na Umoja wa Afrika, uzalishaji wa mafuta ghafi barani Afrika unakadiriwa kuwa karibu mapipa milioni 10 kwa siku, ikiwa ni sawa na asilimia 10 ya uzalishaji wa mafuta ghafi duniani.
Takwimu za Shirika la Nishati la Kimataifa, IEA ambalo hufuatilia biashara za mafuta duniani zinaonyesha kuwa katika uzalishaji wa mafuta wa Mwezi Mei 2025, Nigeria iliongoza kwa mapipa milioni 1.26 kwa siku ikafuatiwa na Libya iliyozalisha mapipa milioni 1.26.
Mwezi huo Gabon ilizalisha mapipa 250,000.
Congo nayo ikawa na 230,000, huku Algeria ikizalisha mapipa 930,000 na Guinea ya Ikweta 60,000 kwa siku. Nchi nyengine barani zinazozalisha mafuta ghafi ni pamoja na Chad, Sudan Kusini, Misri na Angola.
Nchi kama Kenya, na Uganda zipo katika mchakato wa kuanza kuzalisha mafuta.
Mafuta ghafi yanachimbwa kutoka kwenye visima vya ardhini au kwenye maeneo ya pwani na kusafirishwa kwa mabomba au meli za mafuta hadi kwenye vituo vya kusafisha mafuta ambapo yanaweza kugeuzwa na kuwa bidhaa muhimu za mafuta, hasa mafuta na kemikali za viwandani.
Takriban 75% ya mafuta yanayozalishwa katika bara la Afrika yanauzwa nje kama ghafi huku bidhaa nyingi za mafuta zikiagizwa kutoka nje, jambo ambalo linaifanya Afrika kuwa bara pekee duniani ambalo ni muuzaji mkuu wa mafuta ghafi nje ya nchi na pia muagizaji mkuu wa bidhaa za petroli. Saudi Arabia, Falme za Kiarabu, na Kuwait zikiwa wasambazaji wake wakubwa.
Misri kwa mfano inatumia takriban mapipa laki nane kwa siku, Afrika kusini mapipa laki sita, Nigeria laki tano na Algeria laki nne kwa siku. Matumizi haya ni ya juu hasa kwa sababu ya idadi yao ya watu na uwekezaji katika viwanda.
Aidha, pia Afrika imejaaliwa kuwa na kiasi kikubwa cha gesi asilia, ambayo inaweza kupatikana hasa katika mataifa ya Algeria, Tunisia, Libya, Nigeria na Misri.
Asilimia 40 ya ugunduzi mpya wa gesi asilia duniani katika miaka kumi iliyopita ni barani Afrika, haswa Senegal, Mauritania, Msumbiji, Tanzania, miongoni mwa nyengine.
Kwa sasa, zaidi ya 45% ya gesi asilia inayozalishwa barani Afrika inauzwa nje ya nchi na mchango wa gesi asilia barani Afrika katika usawa wa nishati ni mdogo.
Kwa mataifa yanayotoa mafuta kama Nigeria, Angola na Libya, hii inaweza kuwa habari njema kwa muda mfupi.
Bei za juu zinamaanisha mapato zaidi, fedha nyingi za kigeni, na kuchangia katika makadirio makubwa ya bajeti ya taifa.
Lakini ikiwa tu itamaliza changamoto za miundombinu ya muda mrefu, wizi na uwekezaji duni.
Hata hivyo, kwa bara zima la Afrika, taswira hiyo inaashiria hali mbaya zaidi. Nchi kama Kenya, Rwanda, na Afrika Kusini zinategemea sana uagizaji wa mafuta kutoka nje.
Kupanda kwa bei ya mafuta duniani kunamaanisha mafuta yatakuwa ghali zaidi yatakapofika katika nchi zao, bei ya juu ya kusafirisha bidhaa, na hatimaye, familia kulazimika kubana matumizi kutokana na kupanda kwa gharama za maisha.












