Kenya yapigia mfano Uturuki katika uboreshaji wa uwanja wa ndege wa JKIA
AFRIKA
4 dk kusoma
Kenya yapigia mfano Uturuki katika uboreshaji wa uwanja wa ndege wa JKIAUmaarufu na weledi wa Uturuki katika huduma za anga unazidi kuvupa mipaka, huku Kenya ikijaribu kuiga mfano wan nchi hiyo katika kuboresha miundombinu yake.
Muonekano wa juu wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta./Picha:KAA
tokea masaa 10

Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), ulioko jijini Nairobi uko kwenye pilikapilika za maboresho.

Ukiwa umejengwa mwaka 1978, na uwezo wa kuhudumia abiria milioni 2 kwa mwaka, kwa sasa uwanja huo mkubwa nchini Kenya una uwezo wa kuhudumia wasafiri milioni 10.

 "Uwanja huu huwa na pilikapilika nyingi kati ya nyakati za ndege kutua,” anasema Caleb Kositany, Mwenyekiti wa Mamlaka za Viwanja vya Ndege Kenya (KAA), katika mahojiano yake na TRT Afrika.

Kositany, ambaye alikuwa nchini Uturuki hivi karibuni kwa ziara binafsi, anatabanaisha namna uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Istanbul ulivyosheheni yote yanayohitajika kwenye sekta ya usafiri wa anga.

Mwenyekiti huyo wa KAA anaonesha matumaini yake kuwa, labda siku moja JKIA itafuata nyayo hizo hizo.

Uturuki imeibuka kinara wa kuleta mapinduzi kwenye sekta ya usafiri wa anga katika eneo la Afrika Mashariki, wakati ambapo Kenya imeanza kutoa zabuni kwa ajili ya upanuzi wa JKIA.

"Tuna mengi ya kujifunza,” anasema Kositany, akibainisha kuwa hatua kubwa iliyopigwa na Uturuki kwenye sekta ya usalama wa anga ni mfano wa kuigwa kwa Kenya.

"Tumeshavuka lengo la mahitaji ya awali," anasema Kositany akizungumzia michoro ya mwanzo ya JKIA. "Kwa sasa, tunahudumia zaidi ya abiria milioni tisa huku uwezo wetu ukiwa umekwama kwenye milioni mbili."

Kulingana na Kositany, tayari baadhi ya makampuni ya Uturuki yameanza kuulizia fursa kuhusu mradi wa upanuzi wa JKIA.

Ushirikiano huo hautoishia JKIA peke yake, bali utakwenda kwenye uanzishwaji wa viwanda vya nguo chini Kenya.

"Mara nyingi tunaenda kule kujinunulia vitu kama vile nguo nzuri, suti ambazo zinatengenezwa Uturuki," anasema Kositany.

"Tunaangalia uwezekano wa kuleta utaalamu wa kutengeneza nguo nchini Kenya."

Kwa upande mwingine, Kenya inachungulia fursa za uwekezaji katika sekta ya maziwa.

Miradi iliyosimama

Jitahada mbalimbali za kuuboresha uwanja wa ndege wa JKIA, ikiwemo mradi wa Adani, hazikuzaa matunda.

Kwa sasa, KAA inaandaa zabuni kwa ajili ya kuwavutia washirika wapya wa kimataifa kwa kazi hiyo.

Kositany anasisitiza kuwa wanataka uwazi na ukweli kwenye utekelezwaji wa mkakati huo.

"Tunataka mtu aje na pesa mezani. Tukikubaliana leo, basi kazi ianze kesho mara moja," anaeleza.

Mbali na upanuzi huo, KAA pia imelenga kufanya maboresho kwenye eneo la abiria.

Vifaa vya kisasa vya ukaguzi vitaondoa adha ya uvuaji viatu mara kwa mara kwa abiria huku teknolojia ya utambuzi sura, itatumika kuongeza ufanisi.

Uwezo wa Uturuki

Maofisa wa Kenya wanachukua mfano wa mafanikio ya sekta ya usafiri wa anga Afrika Magharibi, kama ulivyofanikishwa na makampuni ya Uturuki.

Mfano mzuri ni Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Blaise Diagne uliopo Senegal na Diori Hamani wa nchini Niger.

Mbali na ukarabati wa viwanja vya ndege, Shirika la Ndege ya Uturuki linaruka na kutua kutoka mataifa mengi zaidi barani Afrika, kuliko mashirika mengine duniani.

Kwa sasa, shirika hilo lina safari 65 katika nchi 41.

Nchini Tanzania, kampuni ya Çelebi ndio inayohusika na usafirishaji wa mizigo, ikifanya kazi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

Kwa Somalia, kampuni ya Favori imekuwepo katika uwanja wa ndege wa Aden Adde kuanzia mwaka 2013.

Mtandao wa kikanda

Ukiwa ni uwanja wa ndege wenye shughuli nyingi zaidi katika eneo la Afrika Mashariki, JKIA imejiwekea lengo la kuhudumia abiria milioni 31, ifikapo mwaka 2055.

Hivi karibuni, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Moi ulioko Mombasa, ulifanyiwa maboresho ili kuongeza ufanisi wake wa kila siku.

Pia vipo viwanja vya ndege vyenye kutuoa huduma mtambuka, kama vile  Eldoret uliopo katika kaunti ya Uasin Gishu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kisumu, ambao nao uliwekwa vifaa vya kisasa vya usalama wa ndege.

"Tunayo mengi ya kufanya. Tunataka Wakenya wafurahie miundombinu bora na Uturuki ni kati ya machaguo yetu kutokana na hatua kubwa waliyopiga katika sekta ya anga," anaeleza Kositany.

 

 

 

CHANZO:TRT Afrika