| Swahili
UTURUKI
2 dk kusoma
Uturuki yalaani Polisi wa Georgia kwa kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya mashabiki wa Beşiktaş
Mawaziri na maafisa mbalimbali wa serikali ya Uturuki wameilaani vikali hatua ya polisi wa Georgia ya kutumia nguvu dhidi ya mashabiki wa klabu ya Beşiktaş wakieleza kuwa hatua hiyo ilikuwa ya kupita kiasi na isiyokuwa na uwiano.
Uturuki yalaani Polisi wa Georgia kwa kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya mashabiki wa Beşiktaş
Shabiki wa Beşiktaş aliyejeruhiwa na polisi anapelekwa hospitalini. / / َAA
 

Mawaziri na maafisa mbalimbali wa Uturuki wametoa matamshi hayo kufuatia tukio la polisi wa Georgia kuingilia kati na kutumia nguvu dhidi ya mashabiki wa Beşiktaş kabla na wakati wa mchezo wa Ligi ya Europa ya UEFA dhidi ya Hapoel Beer-Sheva ya Israel, uliochezwa mjini Batumi, Georgia.

Kwa mujibu wa vyanzo vya Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki vilivyonukuliwa siku ya Alhamisi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan, alifanya mazungumzo ya simu na mwenzake wa Georgia, Maka Botchorishvili, kujadili tukio hilo.

Waziri wa Vijana na Michezo wa Uturuki, Osman Aşkın Bak, alilaani vikali hatua ya vikosi vya usalama vya Georgia, akisema kuwa matumizi ya nguvu dhidi ya mashabiki wa Beşiktaş yalikuwa ya kupita kiasi.

"Tunapinga aina zote za ubaguzi na ukosefu wa haki ambazo haziendani na misingi na maadili ya kimataifa ya michezo. Tutaendelea kutetea kwa dhati haki za michezo ya Uturuki na mashabiki wetu katika kila jukwaa," alisema Bak.

Kwa upande wake, Burhanettin Duran, Mkuu wa Mawasiliano wa Uturuki, alilaani hatua ya polisi na kutoa pole kwa mashabiki walioathirika.

Alisisitiza kuwa kuonesha mshikamano kwa njia za amani na wananchi wa Palestina hakupaswi kutumiwa kama kisingizio cha kutumia nguvu dhidi ya watu.

"Maonesho ya amani ya mshikamano na wananchi wa Palestina hayapaswi kamwe kuwa sababu ya vitendo vya ukatili au matumizi ya nguvu," alisema Duran.

Aliongeza kuwa mwitikio mkubwa zaidi dhidi ya kile alichokitaja kuwa ni ukosefu wa haki waliotendewa mashabiki wa Beşiktaş ulitolewa na klabu mbalimbali maarufu za michezo nchini Uturuki kupitia jumbe zao za mshikamano, huku Beşiktaş yenyewe ikijibu kwa kupata ushindi uwanjani.

Polisi watumia nguvu kupita kiasi

Tukio hilo lilianza baada ya shabiki mmoja wa Beşiktaş kupeperusha bendera ya Palestina, hatua iliyosababisha polisi wa Georgia kuingilia kati.

Polisi walitumia dawa ya pilipili na kumzunguka shabiki huyo, hali iliyochochea mvutano na kusababisha makabiliano zaidi kati ya mashabiki na vikosi vya usalama.

Kutokana na hali hiyo, mwamuzi wa mchezo kutoka Denmark, Morten Krogh, alilazimika kusimamisha kwa muda mchezo huo katika dakika ya 26.

Timu zote mbili zilitakiwa kuondoka uwanjani na kuelekea kwenye vyumba vya kubadilishia nguo wakati hali ya usalama ikidhibitiwa.

Wakati huo, wachezaji wa Beşiktaş walijaribu kuwatuliza mashabiki wao ili kupunguza mvutano na kusaidia kurejesha hali ya utulivu uwanjani.

CHANZO:TRT World and Agencies