| Swahili
ULIMWENGU
2 dk kusoma
Trump: Marekani ina fedha za kuendeleza vita dhidi ya Iran hadi mwisho wa Januari
Trump amesisitiza kuwa Marekani inaweza kusitisha vita hivyo wakati wowote itakapoamua.
Trump: Marekani ina fedha za kuendeleza vita dhidi ya Iran hadi mwisho wa Januari
“Tunaweza kukomesha vita hiyo wakati wowote tunapotaka,” alisema Trump. / / AP
 

Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuwa nchi yake ina fedha za kutosha kuendeleza vita dhidi ya Iran hadi mwisho wa mwezi Januari. Aidha, amesisitiza kuwa anaweza kusitisha mzozo huo wakati wowote atakapoamua.

Katika mahojiano na gazeti la New York Post, yaliyochapishwa Jumanne, Trump pia aliwakosoa wanachama wa Democratic waliopo katika Bunge la Marekani, akionya kuwa jitihada zao za kuweka vikwazo katika operesheni za kijeshi zinaweza kugeuza alichokitaja kuwa ushindi wa Marekani na kuifanya nchi hiyo kuwa katika hali ya kushindwa.

“Watachukua ushindi wa moja kwa moja na kuugeuza kuwa katika hali ya kushindwa,” alisema Trump. Alidai kuwa jeshi la wanamaji la Iran, jeshi la anga na mifumo yake ya ulinzi wa anga vimeangamizwa, huku viongozi wa nchi hiyo wakiondolewa madarakani.

Alipoulizwa iwapo uwezo wake wa kuchukua hatua za kijeshi unaweza kuwekewa mipaka zaidi iwapo wanachama wa Democratic watachukua udhibiti wa Bunge la Marekani mwezi Januari, Trump alisema utawala wake una fedha za kutosha kuendeleza operesheni za kijeshi hadi wakati huo.

“Kwa kiasi kikubwa, hadi kufikia mwisho wa Januari, tuna fedha za kuendesha operesheni hizo,” aliliambia gazeti hilo.

Trump alisisitiza kuwa Marekani inaweza kusitisha vita hivyo wakati wowote itakapoamua, akisema: “Tunaweza kuumaliza vita hivyo wakati wowote tunapotaka.”

Pia alizungumzia uwezekano wa kubadilika kwa mfumo wa utawala nchini Iran, akieleza kuwa jambo hilo “huenda likawezekana”, lakini akasisitiza kuwa si lengo lake kuu.

“Jambo pekee ninalotaka ni kuhakikisha kuwa hawapati silaha ya nyuklia. Sikuwahi kuwa chabiki wala mpinzani wa mabadiliko ya utawala nchini Iran; hilo halijawahi kuwa kigezo changu,” alisema Trump.

CHANZO:Anadolu Agency