Rais wa Nigeria Bola Tinubu amekiri kuwa changamoto za uhaba wa maji na kukatika kwa umeme pia zinaathiri Ikulu, akieleza namna maji yalivyokatika wakati akinyoa katika Ikulu ya mji mkuu wa Abuja.
Tinubu alieleza hayo wakati wa hafla rasmi ya maombi maalum siku ya Jumapili yaliyoandaliwa na Klabu ya Tenisi ya Wayoruba mjini Lagos, ambapo pia aliomba kuungwa mkono kwa kampeni zake za kutaka kuchaguliwa tena kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Akieleza kuhusu tukio hilo la wiki iliopita, rais alisema tatizo hilo lilitokea hata katika Ikulu, inayojulikana maarufu kama Aso Rock.
‘Tutarekebisha hilo’
Aliahidi kushughulikia changamoto za miundombinu nchini, ikiwemo kukatika kwa umeme na usambazaji wa maji.
“Tutarekebisha hilo: hakuna taa, hakuna maji, hakuna umeme, hakuna maendeleo. Ndiyo tumeanza tu. Tunaweza kufanya hilo, na tutafanya kwa ajili ya Nigeria,” alisema.
Kauli hiyo ya Rais imefanya tatizo la muda mrefu la changamoto za miundombinu nchini Nigeria kuangaziwa, hasa kukatika kwa umeme na uhaba wa maji kwa wananchi,ambalo linaendelea kuathiri maeneo ya watu, biashara na taasisi za umma.














